Mkutano wa amani wa ahirishwa Afrika kusini.
24 Machi 2009Waandazi wa Mkutano wa amani nchini Afrika Kusini, wameuahirisha mkutano huo leo kwa muda usijulikana . Sababu ni kuwa, serikali ya Afrika kusini, imemkatalia ruhusa ya kuingia nchini Dalai Lama,kiongozi wa watibeti-hatua ambayo imeongoza kujitoa kabisa mkutanoni mshindi huyo wa Tuzo la amani la Nobel.
Mkutano huu ambao ulikuwa ufanyike ijumaa,ulipanga kuhimiza juhudi za amani kupitia mchezo wa kabumbu kabla Kombe la dunia la FIFA kuanza mwakani nchini Afrika Kusini.
Uamuzi wa kuuahirisha mkutano huu ulitarajiwa baada ya Askofu Desmond Tutu,rais wa zamani wa Afrika kusini FW De Klerk na Kamati ya Nobel ya Norway,wote kutangaza jadharani kwamba wataususia mkutano huo ikiwa serikali ya Afrika Kusini haitaufuta uamuzi wake wa kumkatalia Dalai lama visa ya kuingia nchini.
Irvin Khoza, mwanachama wa kamati ya mkutano huo aliwaambia maripota na ninamnukulu, "Kwavile shabaha ya mkutano huu ni kupigania amani,walioitisha hawataki kuitia kamati ya nishani ya amani ya Nobel katika mfarakano."
Akaongeza kusema kwamba, serikali ya Afrika kusini ,haimpingi Dalai Lama ,lakini kuhudhuria kwake hakutaleta masilahi yoyote ya Afrika kusini.Isitoshe, kutageuza macho nje ya Kombe lijalo la Dunia.
Kwa kweli, serikali ya afrika kusini inadhaniwa haitaki kuiudhi China ,mshirika wake mkubwa .
Msemaji wa rais ameungama jana kwamba, wakuu wa China wamezungumza na serikali ya Afrika Kusini kuhusu ziara ya Dalai Lama ,lakini imekanusha kuwa hiyo ndio sababu ya kumnyima visa.
Rais wa zamani Nelson Mandela, ndie alietia saini barua ya mwaliko kupelekwa kwa Dalai Lama kupitia mkononi mwa Askofu Tutu na De Klaerk.Binafsi Mandela, hakupanga kuhudhuria mkutano huo.Hii ni kwa muujibu wa Wakfu wake.
Mjukuu wake Mandla Mandela,chiefu wa kienyeji katika kijiji atokako mzee Mandela cha Mvezo,mashariki mwa Cape na pia mjumbe wa kamati ya mkutano huu,ameituhumu serikali ya Afrika kusini kuitia dosari heba ya Afrika kusini.
Jamhuri ya watu wa China, ni mmoja wa washirika wakubwa wa kibiashara wa Afrika Kusini. Pia China ni mtiaji raslimali mkubwa wakati huu barani Afrika-bara ambalo linaipatia nayo China mafuta na madini inayohitaji kuukuza uchumi wake.
Wiki iliopita Mfuko wa dala bilioni 1 wa maendeleo ya afrika ulifungua afisi yake ya kwanza barani Afrika, mjini Johannesberg mbele ya mtetzezi wa wadhifa wa urais na mwenyekiti wa chama-tawala ANC ,Jacob Zuma.
Mkasa huu umeibuka wakati wa kuadhimish mwaka wa 50 tangu jaribio la kuasi dhidi ya utawala wa China mkoani Tibet,eneo lenye mamlaka maalumu nchini China na ambalo China, inadai ni sehemu ya milki yake lakini Dalai Lama anadai Tibet ilikua huru kabla kuwekwa chini ya ukoloni wa China.
Muandishi: Ramadhan Ali
Mhariri: M.Abdulrahman