1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa ASEAN waanza Australia

4 Machi 2024

Mataifa 10 ya Kusini Mashariki mwa Asia na Australia yameanza mkutano wa kuzungumzia masuala mbalimbali yanayoihusu kanda hiyo huku kile kinachosemwa kuwa ni "matumizi ya nguvu" ya China ikiwa miongoni mwa ajenda.

Australia Melbourne 2024 | Ferdinand Marcos Jr.
Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Mdogo akihutubia Taasisi ya Lowy wakati wa Mkutano Maalum wa ASEAN-Australia mjini Melbourne, AustraliaPicha: Hamish Blair/AP Photo/picture alliance

Katika mji wa Melbourne nchini Australia, unafanyika mkutano wa viongozi wa mataifa ya kusini mashariki mwa Asia na Australia unaotarajiwa kutoa kauli ya pamoja ya kushutumu kile wanachosema ni "matumizi ya nguvu" katika mizozo ya kikanda, huku pia mjadala kuhusu China na mataifa jirani juu ya eneo la bahari linalozozaniwa ukiwa ni miongoni mwa ajenda kuu. 

Mapema hii leo, mataifa 10 ya kusini mashariki mwa Asia na Australia yameanza mkutano wa pamoja kuzungumzia masuala mbalimbali yanayoihusu kanda hiyo, huku kile kinachosemwa kuwa ni "matumizi ya nguvu" ya China katika kampeni zake za kutanua wigo katika Bahari ya China Kusini yakiwa miongoni mwa ajenda ya awali kabisa kujadiliwa katika mkutano huo.

Soma pia: Wakuu wa ulinzi wa ASEAN wataka mapigano Gaza yakomeshwe

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyeji wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya ndani wa Australia, Penny Wong, amesema "Tunakabiliwa na vitendo vya uvunjifu wa amani na vya kulazimisha ikiwa ni pamoja na tabia zisizo salama baharini na angani, na matumizi ya kijeshi yasiyo na msingi."

"Tunajua kwamba nguvu za kijeshi zinapanuka lakini hatua za kuzuia mzozo wa kijeshi haziko hivyo, na kuna mbinu chache madhubuti za kuepusha hilo," ameongeza Penny Wong.

Waziri huyo aliongeza kuwa ipo haja ya mataifa ya ukanda huo kuchukua jukumu la pamoja ili kuliweka eneo hilo kuwa la amani, utulivu na leye ustawi.

Miito yatolewa kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza

Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim, kushoto, na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese wanafanya mkutano na waandishi wa habari kabla ya Mkutano Maalum wa ASEAN, Melbourne.Picha: Steve Christo/AP Photo/picture alliance

Wakati msimamo wa kambi hiyo kuhusu Bahari ya China Kusini ukionekana kutatuliwa kwa kiasi kikubwa, kulikuwa pia na matarajio ya majadiliano kuhusu masuala nyeti kama vile vita vya Gaza vinavyoendelea huko Mashariki ya Kati.

Asilimia 40 ya Waislam duniani wapo kusini mashariki mwa Asia na mataiafa kama Indonesia na Malaysia, ambayo pia yanashiriki mkutano huu, yanaiunga mkono Palestina katika majukwaa ya kimataifa.

Aidha mataifa mengine ya ukanda huo kama Singapore yakiwa na uhusiano wa karibu mno na Israel, jambo linaloufanya mkutano huo kuwa na mawazo mseto linapokuja suala la kuzizungumzia Israel na Palestina.

Soma pia:  Marekani yasisitiza wito wa kusimamisha mapigano Gaza

Alipoulizwa mtazamo wake juu ya kinachoendelea huko Gaza, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim alisema ''Pengine ili kuepeuka masuala yenye utata kati ya Palestina na Israel ni muhimu tu kwamba kuwepo kwa usitishwaji mapigano na kupatikana kwa misaada ya kiutu."

Mkutano huo wa siku tatu pia unatarajiwa kuangazia ushirikiano wa kiuchumi, huku nchi kama vile Ufilipino na Australia zikitarajia kutafuta mbinu za kuzihami chumi zao dhidi ya China ambayo imekuwa kwenye mvutano na mataifa hayo juu ya eneo la Bahari ya China Kusini.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW