Mashindano ya ushawishi: China na Marekani ndani ya ASEAN
26 Oktoba 2025
Mkutano wa siku tatu wa jumuiya ya Mataifa ya Kusini mwa Asia, ASEAM, unaoanza Jumapili mjini Kuala Lumpur, Malaysia, utajadili ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda, mazingira, maendeleo ya kidijitali, pamoja na amani, usalama na uthabiti wa eneo hilo.
Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi walioalikwa, ambapo atashiriki hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya Thailand na Cambodia, mkataba aliouwezesha baada ya mapigano ya mpaka yaliyodumu siku tano.
Tukio hilo limeonyesha kwa kiasi gani Marekani bado ina ushawishi mkubwa katika eneo la Asia-Pasifiki, hususan katikati ya ushindani unaoongezeka na China.
Mashindano ya kisiasa kati ya Marekani na China yamejikita pia katika suala la Taiwan na Bahari ya China Kusini. China inadai Taiwan ni sehemu yake, huku Marekani ikiunga mkono hali ya sasa ya kisiwa hicho kama demokrasia inayojitawala.
Wakati huo huo, mataifa kama Ufilipino, Vietnam, na Malaysia yameendelea kulalamikia madai ya China juu ya karibu asilimia 90 ya Bahari ya China Kusini kupitia "mstari wa alama tisa” unaokiuka sheria za kimataifa na mipaka ya kiuchumi ya mataifa mengine.
Walaazimika kuchagua upande
Hali hii, pamoja na mvutano wa kibiashara unaoendelea kati ya Washington na Beijing, imezidisha shinikizo kwa nchi za ASEAN ambazo zinajikuta zikiombwa kuchagua upande.
Wataalamu kama Felix Heiduk wa Taasisi ya Ujerumani ya Utafiti wa Masuala ya Kimataifa na Usalama wanasema shinikizo hili linaonekana zaidi katika sekta za biashara, usalama, na teknolojia — kana kwamba ni "mchezo wa ushindi wa upande mmoja.”
Hata hivyo, mataifa mengi ya ASEAN yanajaribu kuepuka kuchagua upande wowote. Utafiti wa jarida The Diplomat unaonyesha baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo wamevunjika moyo na sera za ushuru za Trump, ambazo zimeathiri hata washirika wa karibu wa Marekani.
Aidha, matamshi ya Trump kuhusu udhibiti wa maeneo kama Mfereji wa Panama, Greenland na Kanada yamezua hofu kwamba msimamo kama huo unaweza kuihamasisha China kufanya madai ya ardhi zaidi katika eneo la Asia Kusini Mashariki.
Kwa mujibu wa The Diplomat, hali hii imepelekea kuwepo na mtazamano tofauti kuhusu Marekani katika mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia.
Marekani haitazamwi kama mshirika wa kutegemea
Baadhi ya nchi za ASEAN haziiangalii tena Marekani kama mshirika wa kuaminika — hasa kutokana na ongezeko la msimamo mkali wa China katika eneo hilo, anasema Andreas Ufen, mtaalamu mwandamizi wa Taasisi ya Ujerumani ya Utafiti wa Masuala ya Kimataifa na Kieneo (GIGA) ya mjini Hamburg.
Kulingana na ripoti ya East Asia Forum, jukwaa la kimataifa la sera kuhusu eneo la Asia ya Mashariki, China inadai maeneo ya nje ya mipaka yake na inajenga visiwa bandia kwa matumizi ya kijeshi — hasa karibu na, na juu ya, visiwa vya Spratly na Paracel.
Ripoti hiyo pia inasema China inachimba na kutumia rasilimali katika maeneo yenye migogoro, hatua inayosababisha usumbufu katika usafiri wa baharini.
Nchi wanachama wa ASEAN zinaitikia ukakamavu wa China kwa njia tofauti. Baadhi ya zile zenye uchumi dhaifu hazina budi ila kuvumilia hali hiyo.
"Kwa mfano, Myanmar, Cambodia na Laos zimeegemea kwa karibu zaidi upande wa China, kiuchumi na pia katika sera za usalama na ulinzi,” alisema Heiduk. "Aidha, nchi hizi hazina uhusiano wa karibu wa kijeshi na kiusalama na Marekani.”
Juhudi za kudumisha usawa
Nchi kubwa na tajiri zaidi zinajaribu kudumisha usawa kwa kushirikiana na mataifa yote mawili kadiri zinavyoweza.
Kwa mfano, Ufilipino inashirikiana kwa karibu na Marekani katika masuala ya ulinzi na usalama, kupitia mkataba wa pamoja wa ulinzi uliosainiwa mwaka 1951.
Heiduk anaeleza kuwa ushirikiano huo umekuwa muhimu zaidi kutokana na ongezeko la uwepo wa kijeshi wa China katika Bahari ya China Kusini.
"Hata hivyo, ushirikiano huo wa kijeshi hauizuii Ufilipino kudumisha uhusiano wa karibu wa kiuchumi na China,” Heiduk alibainisha. "China ni miongoni mwa washirika watatu wakuu wa biashara wa Ufilipino na pia mwekezaji muhimu nchini humo.”
"Indonesia wakati mwingine hushirikiana na China, na wakati mwingine na Marekani,” anabainisha Ufen. Kuhusu masuala ya ulinzi na ununuzi wa silaha, Indonesia inaelekea kushirikiana zaidi na washirika wa Magharibi.
"Kwa sababu ikiwa kungetokea mzozo wa kijeshi, kuna uwezekano mkubwa ungekuwa katika Bahari ya China Kusini dhidi ya China,” anaeleza Ufen. Marekani hata hufanya mazoezi makubwa ya kijeshi pamoja na Indonesia.
Hata hivyo, hayo hayaizuii Indonesia kutafuta uhusiano wa kiuchumi na China. "Kiuchumi, Indonesia na China hushirikiana kwa karibu sana,” anasema Ufen.
Mchambuzi wa GIGA, Andreas Ufen, anaongeza kuwa Indonesia pia inajaribu kuepuka kuchagua upande wowote.