1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufungua pazia leo

19 Septemba 2023

Mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa unaanza leo kwenye makao makuu ya umoja huo mjini New York chini ya kiwingu cha mizozo ulimwenguni na kitisho kinachoongezeka cha athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa
Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa MataifaPicha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua News Agency/picture alliance

Wakuu wa nchi na serikali kutoka zaidi ya mataifa 140 duniani wanatarajiwa kuhutubia mkutano huo utakaofunguliwa kwa hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres. 

Hotuba nyingine za leo inajumuisha ile ya rais Joe Biden kwa nafasi yake kama nchi mwenyeji pamoja na ya rais Inácio Lula da Silva wa Brazil, ambaye nchi yake ndiyo kwa jadi hufungua pazia la hotuba za viongozi.

Lula anatazamiwa kuimarisha nafasi ya nchi yake kama kiongozi wa mataifa yanayoendelea.

Mwengine atakayetoa hotuba ni rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba ambaye siku chache zilizopita alikuwa mwenyeji wa mkutano wa kundi la G77 linalojumuisha nchi zinazoendelea duniani pamoja na China.

Rais Recep Tayyip Rdogan wa Uturuki, Volodomyr Zelensky wa Ukraine, rais Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida  ni miongoni mwa wale walio kwenye orodha ya kusimama jukwaani hii leo.

Mivutano kutatiza mwafaka wa ulimwengu kuhusu masuala muhimu 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akihutubia mkutano wa kilele kuhusu malengo ya maendeleo endelevu mjini New York.Picha: Jason Szenes/UPI Photo/newscom/picture alliance

Mivutano baina ya madola yenye nguvu duniani huenda itazuia kupatikana sauti ya pamoja katika kuzikabili changamoto za ulimwengu.

Hata hivyo kulikuwa na ishara ya matumaini hapo jana wakati wa mkutano wa awali uliofanyika kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Nchi wanachama wa umoja huo waliazimia kwa pamoja kuendeleza mipango ya kuyafikia malengo hayo 17 ikiwemo kutokomeza umasikini uliotopea ifikapo mwaka 2030.

Mataifa yanayoendelea nayo yametoa wito wa mageuzi kwenye utaratibu wa sasa unaoongoza dunia ili kuyapiga jeki yatimize lengo la kutokomeza umasikini.

Malengo hayo yalipitishwa na nchi wanachama wa Umoja huo mwaka 2015.

Guterres ataka mpango mbadala kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu 

Mizozo, ukosefu wa ufadhili wa kutosha na athari za mabadiliko ya tabianchi vinazidisha ugumu wa kutekelezwa malengo ya maendeleo endelevuPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito wa kuwepo "mpango mbadala" wa kufikia malengo hayo, baada ya kukiri kwamba ni asilimia 15 pekee ya malengo endelevu ndiyo yamo kwenye mkondo wa kufikiwa kikamilifu ifikapo 2030 huku mengine yanakwenda mrama.

"Malengo ya maendeleo endelevu siyo orodha tu ya kile tunachotaka kutimiza. Yanabeba matumaini, ndoto, haki na matarajio ya watu kote duniani," Guterres aliuambia mkutano huo.

Amesema katika dunia iliyojaa neema, "baa la njaa ni doa kwa ubinaadamu na ukiukaji wa kiwango cha juu wa haki za binadamu".

Kwa upande wake rais  Cyril Ramaphosa aliwaambia waliohudhuria kuwa mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu yanategemea maguezi makubwa duniani kwenye mahusiano ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.