Mkutano wa UNGA waanza rasmi New-York
23 Septemba 2025
Kikao cha viongozi wa ngazi za juu cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa kimefunguwa milango yake Jumatatu katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York.
Kutambuliwa kwa taifa huru la Wapalestina ni miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kugubika mkutano huo wa kila mwaka.
Mkutano huo unafunguliwa kwa hotuba ya katibu mkuu Antonio Guterres,wakati ulimwengu ukishuhudia mataifa mengi ya magharibi barani Ulaya yakitangaza hatua za kulitambuwa dola la Wapalestina.
Mkutano huo unaowakusanya viongozi wakuu wa nchi na serikali unafunguliwa ikiwa ni kipindi tete katika historia ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa huku ulimwengu ukikabiliwa na changamoto mbali mbali za migogoro ya vita kuanzia Gaza hadi Ukraine,kubadilika kwa mtazamo wa Marekani kuelekea ulimwengu, miongoni mwa mengine.
Baada ya hapo jana Jumapili viongozi wa Uingereza,Canada, Australia na Ureno kuchukuwa hatua hiyo hivi leo Ufaransa na Ubelgiji zinatarajiwa kufuata mkondo huo wakati wa mkutano wa viongozi wa ngazi za juu utakaoujadili mgogoro wa Gaza mjini New York.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kuelekea mkutano huu wa leo alionesha kuamini kwamba mataifa mengi zaidi yatatangaza kulitambuwa taifa la Palestina:
"Naamini kwamba zitakuweko hatua za wazi zitakazochukuliwa na mataifa mengi ya ulimwengu za kutambuwa haki ya Wapalestina kuwa na uhuru wao na kutambua kwamba ni lazima liundwe dola la Wapalestina na kutambuliwa kwenye mkutano utakaofanyika Jumatatu. Na vile vile kutoa ujumbe wa wazi kwamba mashambulio yanayofanywa Gaza yanapaswa kusitishwa, na kwamba tunataka vita visitishwe mara moja na mateka wote waachiliwe huru''
Ufaransa na Saudi Arabia zinamatumaini ya kuutumia mkutano wa mwaka huu wa viongozi wa dunia na vita vya kikatili katika Ukanda wa Gaza kuonesha udharura wa kushughulikiwa ombi la kuundwa madola mawili kama suluhu katika mgogoro huo kati ya Israel na Palestina.
Juhudi zinazopendekezwa na mataifa hayo ni pamoja na mpango mpya utakaosaidia hatimae kuundwa dola la Wapalestina katika maeneo yaliyonyakuliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967.
Kadhalika juhudi hizo zinajumuisha pia hatua zitakazochukuliwa na mataifa mengi ya Magharibi za kujiunga na sauti za Ulimwengu za kutangaza kulitambuwa taifa huru la Wapalestina hata kabla ya kuundwa kwake.
Rais Macron akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani cha CBS alisema kwamba kulitambuwa taifa huru la Wapalestina hivi leo ni hatua pekee itakayotowa suluhisho la kisiasa katika hali inayoendelea sasa ambayo inapaswa kuzuiwa.
Wakati rais Macron akitarajiwa kutangaza hatua hiyo ya kulitambuwa taifa la Wapalestina huko NewYork, ndani ya Ufaransa hivi leo tayari bendera za Palestina zinapeperushwa katika majengo ya ofisi za mabaraza ya miji.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani mjini Paris mabaraza ya miji 21 imeshapandisha bendera za kuonesha kulitambuwa taifa huru la Wapalestina,licha ya wizara hiyo kupinga kitendo hicho.
Ndani ya Ukanda wa Gaza Israel inaendelea kufanya mashambulio ikisema inawalenga Hamas na makundi ya kigaidi kote kwenye eneo hulo huku Wapalestina wakiripoti juu ya vifo vya takriban watu 30 hadi kufikia asubuhi ya Jumatatu.
Tangu jana Jumapili jeshi la Israel linafanya mashambulio dhidi ya Gaza City na limesema kwamba zaidi ya Wapalestina 550,000 wameuhama mji huo.