1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Baraza Kuu la UN waingia siku ya tano

23 Septemba 2023

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Azerbaijan, Armenia, Urusi, Mexico, Saudi Arabia, Belarus na Venezuela wanatarajiwa kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

UN-Generalversammlung stimmt über Reparationsantrag für die Ukraine ab
Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Mkutano unaowaleta pamoja viongozi wa dunia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York leo umeingia katika siku ya tano. Hotuba zinazotarajiwa leo hii ni kutoka kwa mawaziri wa mambo ya nje wa Azerbaijan, Armenia, Urusi, Mexico, Saudi Arabia, Belarus na Venezuela. Katika hotuba nyingi hadi sasa kuhusu vita vya nchini Ukraine na uvamizi wake, Urusi hatimaye itapanda kwenye jukwaa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ikiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje, Sergey Lavrov.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov.Picha: Francis Mascarenhas/REUTERS

Kwa upande wao viongozi wa mapinduzi ya Niger wamemlaumu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Atonio Guterres kwa kukwamisha ushiriki wao katika mkutano wa Baraza Kuu la chombo hicho, wamesema haua hiyo inadhoofisha juhudi zozote za kuumaliza mgogoro katika nchi yao. Wanajeshi waasi walimpindua rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26 na wamemzuilia nyumbani pamoja na familia yake.

Soma:Viongozi wa Afrika wahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Mazungumzo ya kurejesha utawala wa kiraia nchini Niger bado hayajazaa matunda, huku utawala huo wa kijeshi ukitaka kuweka kipindi cha mpito cha miaka mitatu. Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imetoa wito wa kurejeshwa mara moja kwa serikali ya rais aliyepinduliwa Bazoum iliyochaguliwa kidemokrasia. Mapinduzi hayo pia yamekosolewa vikali na serikali za Magharibi na mashirika ya kimataifa, kama pamoja na Umoja wa Mataifa.

Rais wa Niger aliyepinduliwa Mohamed BazoumPicha: Evelyn Hockstein/Pool/File Photo/REUTERS

Wakati huo huo kandoni mwa mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkuu wa Mpango wa Mazingira wa umoja huo Inger Andersen amesema uzalishaji wataka za plastiki unaongezeka duniani kote na kusababisha uchafuzi zaidi wa mazingira. Mkuu wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Inger Andersen ametoa wito kwa ulimwengu kufikiria upya kuhusu jinsi binadamu anavyotumia plastiki.

Kushoto: Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Inger Andersen alipohudhuria mkutano wa mazingira nchini Sweden.Picha: Jessica Gow/TT NEWS AGENCY/REUTERS

Katika kipindi cha wiki nzima wakati mikutano inapoendelea, waandamanaji wamekusanyika kwenye eneo hilo la mkutano lililowekewa vizuizi kupaza sauti zao kuhusu dhuluma katika nchi zao. Maandamano kama hayo yanatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa mkutano katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Vyanzo: AP/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW