1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Bayoanuwai COP15 wafunguliwa Canada

7 Desemba 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyatolea wito mataifa yanayoshiriki mkutano wa kimataifa wa bayoanuwai kufanya suluhu na maumbile yasili, na kufikia makubaliano thabiti ya kulinda bayoanuwai ya dunia.

Monarch Butterfly
Picha: Creative Touch Imaging Ltd./NurPhoto/picture alliance

Huku kukiwa na onyo kwamba bayoanuwai inapungua kwa kasi ya kutisha, viongozi wa mazingira wanakusanyika mjini Montreal ili kukubaliana juu ya hatua zinazolenga kuboresha mifumo ya ekolojia ya ardhini na baharini na kukusanya mabilioni ya dola kufadhili juhudi hizi za uhifadhi.

Wajumbe kutoka mataifa takribani 190 watakutana kwa karibu wiki mbili, kuanzia leo Jumatano, kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayoanuwai, au COP15, kukamilisha mfumo wa kulinda asilimia 30 ya ardhi ya dunia na maeneo ya bahari kufikia mwaka 2030.

"Tunapigana vita dhidi ya asili," Guterres alisema mjini Montreal siku ya Jumanne kwenye sherehe za ufunguzi wa mkutano huo. "Mkutano huu unahusu kazi ya dharura ya kuleta amani.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres amewataka washiriki wa COP15 kushiriki jukumu la dharura la kufanya amani na maubile ya asili.Picha: Mark J. Sullivan/ZUMA/IMAGO

"Tunachukulia asili kama choo. Na hatimaye, tunafanya hivyo kujiua kwa njia ya uwakala,” alisema.

Soma pia: WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani

"Kwa sababu upotevu wa maumbile na bayoanuwai unakuja na gharama kubwa ya kibinadamu. Mkutano huu ni fursa yetu ya kukomesha tabia hii ya uharibifu, kutoka mafarakano hadi maelewano, na kutumia matarajio na hatua zinazodai changamoto.

"Hakuna visingizio. Hakuna ucheleweshaji. Ahadi zilizotolewa lazima ziwe ni ahadi."

Malengo makubwa

Hivi sasa, asilimia 17 ya nchi kavu na asilimia 10 ya maeneo ya bahari yanalindwa.

Mfumo unaopendekezwa pia unatoa wito wa kupunguza kiwango cha uanzishaji na uanzishwaji wa spishi vamizi kwa asilimia 50, kupunguza matumizi ya viuatilifu kwa nusu na kuondoa utupaji wa taka za plastiki.

Soma pia: Mkataba wa ulinzi wa bahari wapigiwa debe

Malengo hayo ambayo ni makubwa zaidi kuliko yale ya awali ambayo mengi yameshindwa kufikiwa - yanatarajiwa kuwa kiini cha mjadala wa mkutano huo.

Suala jengine litakalokuwa na umuhimu ni fedha, huku mataifa yanayoendelea yakitazamiwa kushinikiza ahadi muhimu za kifedha kabla ya kutia saini makubaliano yoyote.

Rasimu ya mfumo huo inatoa wito wa kuongeza dola bilioni 200 au asilimia 1 ya Pato Jumla la Taifa kwa ajili ya uhifadhi ifikapo mwaka 2030.

Utoaji wa gesi chafu unatajwa kuwa moja ya visababishi vya kutoweka kwa bayoanuwai.Picha: K. Fitzmaurice-Brown/blickwinkel/picture alliance

Dola nyingine bilioni 500 kila mwaka zitakuja kutokana na kuondoa suala nyeti la kisiasa la ruzuku ambalo hufanya chakula na mafuta kuwa nafuu katika maeneo mengi.

Soma pia: Uwindaji haramu tishio kwa wanyamapori

Mabadiliko ya tabianchi pamoja na upotevu wa makazi, uchafuzi wa mazingira na maendeleo vimeathiri zaidi bayoanuwai duniani, huku makadirio ya mwaka wa 2019 yakionya kwamba spishi milioni moja za mimea na wanyama zinakabiliwa na kitisho cha kutoweka ndani ya miongo kadhaa - kiwango hiki cha hasara kikiwa  juu mara 1,000 zaidi ya ilivyotarajiwa.

Mkutano huu wa Umoja wa Mataifa unakuja chini ya mwezi mmoja baada ya nchi kukutana nchini Misri, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kukubaliana kwa mara ya kwanza kuzilipa nchi maskini kwa uharibifu uliosababishwa na sayari inayozidi kukumbwa na ongezeko la joto.

Chanzo: Mashirika