1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Biashara kati ya Asia na Afrika umefunguliwa Tokyo, Japani.

Erasto Mbwana1 Novemba 2004

Mkutano mkuu wa siku mbili wa Biashara na Vitega Uchumi kati ya nchi za Asia na Afrika, unaojulikana kama TICAD, umefunguliwa rasmi leo mjini Tokyo, Japani. Mkutano unafadhiliwa na nchi hiyo, Benki Kuu ya Dunia, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.

Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.
Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.Picha: AP

Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, akizungumza kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesema kuwa bara la Afrika, lenye wakazi wapatao zaidi ya millioni 750 ni tajiri sana kwa rasili mali zake ambazo zinaweza kuwafaa wawekezaji wa Kiasia.

Ameuambia mkutano, wenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mabara haya mawili, "Mageuzi yakiwa yanapamba moto Afrika, bara hili lina rutuba na vitega uchumi vitazaa matunda mazuri."

Kiongozi wa Nigeria, akitoa mwito wa kuanzishwa kwa Kituo cha Vitega uchumi na Biashara kati ya Japan na Afrika na kuanzishwa kwa shirika jipya la vitega uchumi vya Kiasia barani Afrika amesema, "Serikali zilizo rafiki zinapaswa kuzisaidia sekta zao za kibinafsi ili ziweze kujitegemea kivitega uchumi."

Rais Obasanjo amemaliza hotuba yake kwa kusema, "Biashara na vitega uchumi vya watu binafsi kutoka Asia vitasaidia sana katika kupiga jeki ukuaji wa kiuchumi barani Afrika."

Kiongozi wa Nigeria ni miongoni mwa Viongozi wakubwa wa Ushirikiano mpya wa maendeleo barani Afrika (NEPAD). Mpango ulioasisiwa na Afrika Kusini na nchi nyingine za Kiafrika kwa madhumuni ya kuboresha uchumi na mageuzi ya kisiasa na badala yake nchi zinazoendelea zipatiwe vitega uchumi.

Rais Obasanjo hata hivyo amesema kuwa kazi kubwa bado inahitajiwa kufanywa katika kiwango cha serikali kwa madhumuni ya kutilia mkazo imani ya kibiashara.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amesema kuwa Afrika ina fursa kubwa ya vitega uchumi katika miundo mbinu wakati bara hilo likiendeleza haraka kukua kwa miji yake na kuboresha huduma za umeme, bandari na reli.

Ametilia mkazo kwa kusema, "Zaidi ya miaka kumi iliyopita, uwezekano wa kuwekeza vitega uchumi barani Afrika umevurugwa na hali tete ya kisiasa na usalama katika baadhi ya nchi. Hata hivyo hali hiyo inaanza kubadilika haraka."

Waziri Mkuu wa Japani, Junichiro Koizumi, katika hotuba yake ya ufunguzi amesema kuwa Afrika inaweza kujifunza kutoka Asia.

Amesema, "Katika nusu karne iliyopita, uchumi wa Asia umekuwa kwa haraka sana isivyotarajiwa na kupewa jina la "Muujiza wa Mashariki mwa Asia."

Koizumi amesema, "Kusema kweli huo haukuwa muujiza isipokuwa matunda ya judi za kazi za watu wa Asia. Lengo la ushirikiano kati ya Asia na Afrika ni kugawana na kutumia ujuzi wa Asia kwa ajili ya maendeleo ya Afrika."

Zaidi ya nusu ya bidhaa za Afrika zinazopelekwa nchi za nje, zenye thamani ya Dollar Billioni 130 kwa mwaka, zinauzwa katika nchi za Umoja wa Ulaya, asili mia 19 zinakwenda Marekani na asili mia 16 katika nchi za Asia. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Lakini ingawaje ni hivyo, bidhaa zinazopelekwa Asia, zimezidi kuongezeka kwa asili mia 10 kila mwaka kutoka mwaka 1990 mpaka 2001.

Mkurugenzi wa Sekta za Kibinafsi na Maendeleo ya Miundo Mbinu barani Afrika wa Benki Kuu ya Dunia, Michel Wormser, amesema kuwa Afrika inapaswa kuboresha mazingara yake ya kibiashara.

Amesema, "Asia inapaswa kufungua masoko yake zaidi kwa bidhaa zinazotoka Afrika. Ni vigumu kwa Afrika kusafirisha bidhaa nyingine zilizo muhimu isipokuwa ndogo ndogo."

Mkutano wa Tokyo, unaohudhuriwa na Maafisa mia moja kutoka nchi 50 za Kiafrika, 14 za Asia na mashirika ya kimataifa yapatayo 20, unafuatilia ule wa tatu uliofanywa mwaka wa jana.

Mikutano ya TICAD inatokana na juhudi za Wajapani iliyozinduliwa mwaka 1993 kwa lengo la kutafuta ungaji wa kimataifa katika maendeleo ya Afrika na imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka mitano.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW