Mkutano wa biashara za kimataifa nchini Uchina
13 Julai 2005Wakati nchi tajiri na maskini zinatofautiana sana katika suala la kupunguza ruzuku, baadhi ya mawaziri wanadhani tatizo hili litaingilia mkutano muhimu wa nchi 148 wanachama wa shirika la biashara duniani, WTO,uliopangwa kufanyika mwezi Disemba mjini Hong Kong.
Kuna wanaodhani kwamba mkutano utakaofanyika Hong Kong ni nafasi ya mwisho ya kufikia makubaliano. Baada ya hapo kutakuwa na mwaka moja wa kujadili juu ya makubaliano hayo, ambayo Benki ya Dunia imesema yatawatoa mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini kwa kukuza biashara.
Waziri Mkuu mdogo wa Australia, Mark Vaile, amesema kama hawatafikia makubaliano sasa na kusubiri hadi mkutano wa Hong Kong, basi mpango wote uko hatarini.
Mpango huu juu ya biashara za kimataifa ulitakiwa umalizike mwaka wa 2004. Sasa mawaziri wana mpango wa kuumaliza ifikapo mwisho wa mwaka wa 2006. Itakua zaidi ya miaka mitano tangu uanzishwe kwenye mji mkuu wa Qatar, Doha.
Waziri wa kilimo wa Marekani, Mike Johanns, amesema kuna hali ya kuharakisha mambo, na kila mtu anaona jambo hilo. Pia wanajua wana muda mchache hadi mkutano wa Hong Kong uanze.
Jambo lingine linalofanya kuwepo hali ya kuharakisha ni kwamba, serikali ya Marekani iko mbioni kuishughulikia sheria mpya ya kilimo nchini humo, ambayo inahitaji kujumuisha makubaliano ya kupunguza ruzuku yanayo jadiliwa hivi sasa.
Waziri Vaile, akizungumza na wandishi wa habari, alisema kama makubaliano hayo hayatajumuishwa katika sheria hiyo, basi wasahau suala la kujadili biashara za kimataifa kwa miaka mitano au saba ijayo. Kwa hiyo, mkutano wa Hong Kong utaamua kama watapata au watakosa mafanikio.
Suala la kilimo ndilo la msingi katika majadiliano haya, sababu nchi maskini zimelalamika kwamba ushuru mkubwa wa nchi tajiri, wa kuingiza bidhaa ndani ya nchi, pamoja na ruzuku wanazowapa wakulima wao, zinawafanya wabaki maskini na kuwazuiwa wakulima wao kuuza bidhaa zao katika soko la dunia kwa faida.
Mawaziri walifikia hatua muhimu jana baada ya kukubali pendekezo la utaratibu wa kupunguza ushuru wa kuingiza bidhaa nchini, kutoka kwa kikundi cha nchi zinazoendelea 20, kikiongozwa na Brazil. Hatua hii iliwasaidia kujadili biashara za kilimo, baada ya kuwepo kwa kipindi cha miezi kadhaa cha kutoelewana.
Waziri Vaile alifurahi kuona Marekani na Jumuiya ya Ulaya zikishiriki vyema, lakini alikikosoa kikundi cha nchi 10 tajiri, zikiwemo nchi ya Uswisi, Japani na Korea Kusini, kwa kulikataa pendekezo hilo.
Alisema jambo hili linasikitisha na linapinga wito uliotolewa na viongozi wa kikundi cha nchi 8 tajiri, baada ya mkutano wao wa hivi karibuni, wa kutaka kujumuisha nchi zote katika biashara za kimataifa.
Mkutano huo, unaofanyika katika mji wenye bandari, unahudhuriwa na mawaziri zaida ya 30 kutoka nchi tajiri na maskini. Walianza kujadili masuala ya kilimo na kuendelea na masuala ya ushuru na huduma za viwanda.
Waziri wa biashara wa Uchina Bo Xilai ameliambia shirika la habari la Reuters mazungumzo yalikuwa mazuri na kila upande ulikuwa makini.
Nchi ya Pakistani iliwakilisha mpango unaolenga kuunganisha nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea katika utaratibu utakaofuatwa wa kupunguza ushuru wa bidhaa za viwanda.
Nchi tajiri zinashinikiza ili zipewe nafasi kubwa zaidi katika masoko yanayokuwa kama ya Brazil na India. Kwa upande mwingine nchi maskini zinataka kulinda sekta zake zinazokuwa na hazitaki kufikia makubaliano yoyote hadi wahakikishiwe kwamba nchi tajiri zitawajumuisha katika soko la kilimo.
Waziri wa biashara wa India, Kamal Nath, amesema wawakilishi watajadili na kujaribu kufikia makubaliano, lakini tofauti katika malengo yao ni zile zile za tangu mwanzo.