1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa BRICS: Putin akutana na viongozi mbalimbali

23 Oktoba 2024

Mkutano wa 16 wa kilele wa jumuiya ya BRICS ulioanza Jumanne mjini Kazan nchini Urusi unatarajiwa kupitisha maazimio muhimu kuhusu ushirikiano wa kifedha utakaokwepa mfumo wa SWIFT unaotawaliwa na Marekani.

 Putin katika mkutano huo wa kilele wa BRICS mjini Kazan, Urusi
Rais wa Urusi Vladimir Putin katika mkutano huo wa kilele wa BRICS mjini Kazan, UrusiPicha: Alexander Nemenov/Pool via REUTERS

Mshauri wa mambo ya nje wa Kremlin Yuri Ushakov ameutaja mkutano huo kuwa tukio kubwa zaidi la kidiplomasia kuwahi kuandaliwa na Urusi. Nchi 36 zimehudhuria mkutano huo wa BRICS, huku zaidi ya wakuu wa nchi wapatao 20 wakiwasili katika mji wa Kazan.

Baada ya chakula cha jioni, rais Putin alikutana kwa mazungumzo na rais wa Misri Abdelfattah al-Sisi ambaye alipongeza uungaji mkono wa Urusi kwa miradi ya kiuchumi ya Misri, ikiwemo kinu cha nyuklia cha Dabaa kwenye pwani ya Mediterania.

Rais wa China Xi Jinping alifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Putin na walizungumzia kuhusu mzozo wa Ukraine pamoja na mahusiano kati ya nchi wanachama wa BRICS na mataifa ya magharibi. Xi amemwambia Putin kuwa ulimwengu uko katika hali ya sintofahamu lakini urafiki wao wa kimkakati utadumu hadi kwa vizazi vijavyo.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitri Peskov amesema kwa kuwa mataifa ya magharibi yanashambulia maslahi ya Urusi na China, ni wazi kwamba viongozi hao wawili walikuwa na mengi ya kuzungumza na kusisitiza kuwa Moscow na Beijing zina mtazamo sawa linapokuja suala la siasa za kimataifa.

Rais wa China Xi Jinping(kushoto) akisalimiana na rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amemuambia mwenyeji wake kwamba Afrika Kusini inathamini mno mahusiano ya dhati baina ya mataifa yao mawili, huku akisisitiza kuwa Putin ni rafiki na mshirika wa kweli kwa Afrika Kusini tangu zama za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alithubutu kumuambia Putin kuwa mzozo wake na Ukraine unapaswa kumalizwa kwa njia ya amani na kwamba India inaweka kipaumbele kwenye ubinaadamu, na iko tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika.

Soma pia: Modi amuambia Putin akaye kitako na Zelensky

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula Da Silva ambaye hakuhudhuria mkutano huo wa BRICS baada ya kupata ajali akiwa kwenye makazi yake huko Brazilia, kwa sasa anaendelea vyema baada ya kujeruhiwa kichwani mwishoni mwa juma. Rais huyo mwenye umri wa miaka 78 na ambaye taifa lake ni mojawapo wa waanzilishi wa BRICS alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin.  Kutokana na ushauri wa madaktari, Lula alighairi safari yake iliyopangwa kwenda Urusi lakini ofisi yake ilisema kwamba atashiriki mkutano huo kwa njia ya video.

Lengo kuu la mkutano huo wa kilele wa BRICS

Putin amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuanzisha mfumo mbadala wa kifedha ili kuleta ushindani kwa mfumo wa SWIFT, ambao miamala yake ya kimataifa inadhibitiwa na mataifa ya Magharibi. Benki nyingi za Urusi ziliondolewa kwenye mfumo huu baada ya uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akisalimiana na rais Putin wa UrusiPicha: Alexander Nemenov/Pool via REUTERS

Wakati mkutano huo wa BRICS ukiendelea nchini Urusi, DW imezungumza na Theresa Fallon, mwanzilishi na mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo kuhusu Asia Ulaya na Urusi (CREAS) kilichopo mjini Brussels, Ubelgiji amesema lengo kuu la kundi hilo, haswa kwa mataifa ya Urusi na China, ni kujidhihirisha wazi kama washindani wakuu au hata mbadala wa mfumo unaosimamia siasa za kilimwengu.

Wachambuzi wengine wanasema, hatua ya Kremlin kuwa mwenyeji wa mkutano huu, inakusudia kuonesha kwamba Marekani na washirika wake wa Magharibi wameshindwa katika azma yao ya kuitenga Urusi kutokana na vita vyake nchini Ukraine, lakini pia unadhihirisha kuwa Urusi bado ina washirika na marafiki kote duniani.

Wanachama waanzilishi wa BRICS ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Mataifa mengine tayari yamejiunga na jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na Umoja wa Falme wa Kiarabu, Misri, Ethiopia na Iran. Saudi Arabia, ambayo ilialikwa kuwa mwanachama kamili, hadi sasa haijaeleza msimamo wake ulio wazi, huku Argentina ikiamua kujiondowa.

Wakuu wa mataifa wakutana Kazan kwenye BRICS

01:42

This browser does not support the video element.

Mataifa ya Uturuki, Azerbaijan na Malaysia wametuma rasmi maombi ya kuwa wanachama, huku mataifa mengine kadhaa yakionyesha nia ya kujiunga na Jumuiya hiyo. Mkutano wa BRICS ulioanza jana Jumanne na kuwakusanya viongozi mbalimbali wa dunia akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, utamalizika siku ya Alhamisi (24.10.2024).

(Vyanzo: DPAE, AP, AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW