1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

BRICS yamalizika, China yaahidi ushirika zaidi na Afrika

25 Agosti 2023

Rais wa China Xi Jinping amesema ushirikiano thabiti kati ya China na Afrika katikati ya kile kinachoshuhudiwa sasa kimataifa ni muhimu, na hasa katika kulinda maslahi yao halali ya maendeleo.

Südafrika Johannesburg | BRICS-Gipfel | Pressekonferenz
Picha: Sergei Bobylev/dpa/picture alliance

Mkutano wa kilele wa kundi la BRICS linalokutanisha mataifa yanayoinukia kiuchumi umemalizika jana mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kushuhudia mafanikio makubwa na ya kihistoria ikiwa ni pamoja na kundi hilo kuyapatia uanachama mataifa sita. 

Rais wa China Xi Jinping amesema ushirikiano thabiti kati ya China na Afrika katikati ya kile kinachoshuhudiwa sasa kimataifa ni muhimu, na hasa katika kulinda maslahi yao halali ya maendeleo, huku akitoa wito wa juhudi za pamoja katika kujenga jamii itakayoendelea kwa pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna taifa litakaloachwa nyuma.

Alitoa matamshi hayo katika hotuba yake kwenye mjadala wa BRICS-Africa Outreach na Brics Plus Dialogue, iliyofanyika pembezoni mwa mkutano huo wa 15 wa kilele. Aidha ameahidi kuanzisha mkakati wa kusaidia sekta za viwanda na kilimo barani humo ili kuweza kuendana na wakati.

Kwenye majadiliano hayo aidha, rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitumia wasaa huo kusisitiza juu ya umuhimu wa eneo huru ya biashara barani Afrika ili kuwa na uwezo wa kuleta matokeo chanya kwenye sekta zote za uchumi wa Afrika baada ya eneo hili kuanza kazi kikamilifu

Mkutano wa BRICS uliongozwa na wakuu wa mamatifa waasisi China, Afrika Kusini, Brazil na India.Picha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Ramaphosa alisema "Mahusiano yetu na China yatalenga kuhamasisha matokeo yatakayofaidisha pande zote, kwa kuzingatia pia mradi muhimu ambao tumeuanzisha ambao ni Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika ambalo linatarajiwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa chumi zetu."

Katika hatua nyingine, waziri wa fedha wa Afrika Kusini amesisitiza kwamba kundi hilo halitaachana na mifumo ya kimataifa ya malipo ya fedha ikiwa ni pamoja na SWIFT, wakati linapoangazia kuanzisha mfumo wake unaotarajiwa kuimarisha biashara itakayotumia sarafu zao.

Soma Zaidi:Benki ya BRICS inaweza kusaidia miradi ya kukabiliana na changamoto barani Afrika 

Mkutano huo wa siku tatu mjini Johannesburg, ulimalizika jana Alhamisi, na viongozi walisema watawaomba mawaziri wao wa fedha kuangazia suala la kutumia sarafu za ndani, mifumo ya malipo pamoja na mitandao na kuwapa mrejesho baada ya mwaka mmoja.

Mkutano huo wa kilele uliongozwa na rais Ramaphosa wa Afrika Kusini, Xi Jinping wa China, Luizi Inacio Lula da Silva wa Brazil na waziri mkuu wa India Narendra Modi. Rais wa Urusi Vladimir Putin alihudhuria kwa njia ya mtandao. Zaidi ya wakuu 60 wa serikali na mataifa yanayoendelea pia walihudhuria.

Soma Zaidi: BRICS yakubali wanachama wapya sita