1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa COP29 kufunguliwa Jumatatu, Baku

10 Novemba 2024

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock atahadharisha juu ya kitisho cha majanga duniani, akitaja vimbunga hatari, ukame, mafuriko na joto kali.

Mkutano wa kilele wa mazingira COP29
Mkutano wa kilele wa mazingira COP29Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu mazingira unafunguliwa Jumatatu mjini Baku nchini Azerbaijan na tayari waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amegusia juu ya kitisho cha majanga duniani, akitaja vimbunga hatari, ukame, mafuriko na joto kali.Soma pia: Papua New Guinea yatangaza kususia mkutano wa COP29

Picha: Jörg Blank/dpa/picture alliance

Baerbock ambaye pia ni kiongozi wa chama cha walinzi wa mazingira nchini Ujerumani amesema mgogoro wa mazingira ni changamoto kubwa ya kiusalama inayoshuhudiwa hivi sasa.

Wajumbe kutoka mataifa kiasi 200 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo wa kilele wa mwaka huu wa COP29 utakaoendelea hadi Novemba 22.

Matrillioni yanahitajika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Mataifa yanayoendelea na mashirika ya wanahakarati wa kutetea mazingira wanatarajia nchi zilizoendelea kiviwanda kukusanya kiasi dola Trilioni moja kila mwaka kusaidia juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kiwango hicho kikiwa ni mara 10 zaidi ya kile kilichoafikiwa kwa sasa cha dola bilioni 100.

Wakati mabadiliko ya tabia nchi ya yakisababisha majanga ya hali ya hewa yasiyokwisha katika maeneo mbali mbali ya dunia,nchi zinahangaika kutafuta namna ya kuishi na ukweli huo,zikijiandaa kuwa katika nafasi nzuri ya kuhimili vimbunga vikali,mafuriko,joto kali,ukame na moto wa nyika.

COP29 mjini BakuPicha: Jakub Porzycki/NurPhoto/picture alliance

Na yote haya yatahitaji mabilioni ya dolla.

Taasisi kubwa za fedha duniani zinazosimamiwa na fedha za walipa kodi ndio vyanzo vikubwa vinavyoongezeka kwa kasi kuwa wafadhili wa miradi ya kimazingira kwa mataifa yanayoendelea duniani. Na mabenki hayo ni machache ulimwenguni mojawapo ni benki ya dunia.

Soma pia: Guterres: Athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwaBenki hizi ndizo zilizokuwa chanzo kikubwa, mwaka 2022 ulimwengu ulifikia lengo lililowekwa na mataifa  mnamo mwaka 2009 la kutolewa dola bilioni 100 kila mwaka kwa mataifa yanayoendelea kushughulikia miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwahivyo katika mkutano wa Azerbaijan unaofunguliwa Jumatatu,wa Cop29 viongozi wa dunia  wanatarajia kujadili jinsi ya kutafuta matrilioni ya dola kusimamia miradi ya mazingira.

Mafuriko UhipaniaPicha: Bruna Casas/REUTERS

Shirika  lisilokuwa la kiserikali la sera kuhusu mazingira linaloendesha shughuli za utafiti linakadiria kwamba ulimwengu unahitaji kiasi mara tano ya fedha zinazotolewa sasa kila mwaka kusimamia miradi ya kulinda mazingira, ili kuzuia viwango vya joto visipindukie kiwango cha nyuzi 1.5 Celsius.

Afghanistan kwa mara ya kwanza nayo itashiriki mkutano wa Baku kwa mujibu wa shirika lake la ulinzi wa mazingira NEPA,hii ikiwa hatua muhimu kwa taifa hilo,kwasababu itakuwa ni mara ya kwanza kwa ujumbe wa taifa hilo kualikwa mkutano huo wa kilele tangu Taliban iliporudi madarakani Agosti 2021.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW