Mkutano wa COP29 waingia kipindi kigumu cha majadiliano
20 Novemba 2024Shinikizo limeongezeka leo Jumatano kwa mataifa tajiri kutoa ahadi ya kuchangia dola Trilioni 1 kila mwaka kuyasaidia mataifa masikini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wawakilishi wa nchi zinazoendelea kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP29 uaofanyika mjini Baku, Azerbaijan wanasema wenzao kutoka mataifa tajiri hawaonesha nia ya kutaja kiwango walicho tayari kukikotoa.
Soma pia: Tofauti zaibuka katika mkutano wa COP29
Mkwamo huo unashuhudiwa ikiwa zimebaka siku mbili kabla ya kumalizika kwa mkutano wa COP29.
Akizungumza na waandishi habari, mjumbe wa Umoja wa Ulaya kuhusu mabadiliko ya tabianchi Wopke Hoekstra amesema majadiliano yameingia hatua ngumu wakati muda unayoyoma.
Nchi masikini zinazitaka zile tajiri zisaidie gharama za kukabaliana na taathira za kupanda kwa joto duniani, lakini mataifa hasa ya Ulaya yanataka orodha ya wachangiaji itanuliwe kuzijumuisha nchi kama China na madola tajiri ya mashariki ya kati.