Mkutano wa COP30 na umuhimu wake huko Brazil
10 Novemba 2025
Kongamano hilo la kila mwaka linafanyika mjini Belem ulio makao ya msitu wa mvua wa Brazil na msingi wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi,UNFCCC uliotiwa saini miaka 33 iliyopita.
Brazil ilikuwa mwenyeji wa kongamano la mazingira na maendeleo la Rio miongo mitatu iliyopita. Kwa mwaka huu,Brazil ilisisitiza kuwa mkutano huo wa kilele utarejea kwenye mizizi yake ili kuwatambua walio hatarini zaidi yakiwemo makundi ya jamii za kiasili ambao wanaishi kwenye msitu wa mvua na baadhi yao wanashiriki vikaoni.
Brazil inawarai washirika kufanyia kazi ahadi walizotoa kama zile za kongamano la COP28walipoahidi kupunguza na hatimaye kuacha matumizi ya nishati ya visukuku mfano makaa ya mawe,mafuta na gesi asili inayotoa gesi za kaboni zinazochafua mazingira, na badala yake kuunda aina zilizo endelevu.Kongamano la COP 30 ni la kwanza kuwahi kuafiki kuwa lengo la awali la kupunguza viwango vya joto kwa nyuzi 1.5 Celsius halijatimizwa.
Kwa upande wake, Brazil iliamua kuandaa mkutano huo kwenye eneo la msitu wa Amazonia mjini Belem kwa nia ya kuukumbusha ulimwengu umuhimu wa misitu ambayo inalengwa na wafanyabiashara wa kukata magogo na walio kwenye sekta ya madini, kilimo na uchimbaji wa mafuta, makaa ya mawe na gesi.
Aghalabu serikali nyingi huwakilishwa vikaoni,na mataifa mengi yaliyo na masuala yanayoshabihiana huzungumza kwa kauli moja.Baadhi ya mataifa yanayopaaza sauti ni yale ya visiwa ambayo yanakabiliana na hatari ya kudidimia kwani kina cha maji ya bahari kinaongezeka.
Kadhalika,mataifa wanachama wa kundi la G77 yanayoendelea na China, pamoja na kundi la mataifa ya Afrika na lile la BASIC linalozileta pamoja nchi za Brazil,Afrika Kusini, India na China. Ifahamike kuwa Marekani iliyotangaza kujiondoa kwenye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia ya nchi,imejitenga na majukumu ya uongozi.
China, Brazil na mataifa mengine yamechukua hatamu na kujaza pengo hilo.
Kongamano hilo la kila mwaka linajulikana kama COP, kwa maana ya mkutano wa washirika waliotia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1992 wa mabadiliko ya tabianchi.
Mkataba huo wa UNFCCC,unalenga kuzileta pamoja nchi kupambana kwa kauli moja na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoandama mataifa yote. Makubaliano hayo pia yaliridhia maazimio ya pamoja ila wajibu unaotofautiana ukizingatia kuwa mataifa tajiri ndiyo yaliyo na mchango mkubwa kwenye gesi zinazoongeza viwango vya joto kwahiyo kubeba mzigo mkubwa zaidi wa kusaka suluhu.
Kwa mwaka huu,mambo ni tofauti kwani wafadhili walikutana mjini Sao Paulo na viongozi wa kitaifa wanakutana mjini Rio di Janeiro.Viongozi wa kimataifa walikutana mjini Belem kabla ya vikao kuanza rasmi tarehe 10 hadi 21 mwezi huu wa Novemba, imani ikiwa ni kuyapa nguvu.
Katika wiki ya kwanza wataalam wa nchi mbalimbali wanawasilisha hoja zao na mada kuu. Mawaziri watajiunga nao katika wiki ya pili ili kujadili maamuzi ya mwisho yakiwemo ya kiufundi na kisheria. Baada ya hapo, majadiliano ya kina yanafanyika kabla ya kongamano kukamilika ila mitazamo hutofautiana hadi dakika ya mwisho.