1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa COP30 wang'oa nanga Brazil bila Marekani

Sylvia Mwehozi DPA, Reuters, AFP
11 Novemba 2025

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira wa COP30 umefunguliwa jana katika mji wa Brazil wa Belem huku wito ukitolewa kwa ulimwengu kuendeleza mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani bila uwepo wa Marekani.

Brazil Belém 2025 | Rais wa Brazil Lula da Silva akitoa hotuba kwenye sherehe za ufunguzi wa COP30
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva akifungua mkutano wa COP30Picha: Pablo Porciuncula/AFP

Takriban wajumbe 50,000 wanakusanyika kwa ajili ya mkutano wa wiki mbili wa COP30 huko Belem, jiji kuu lenye joto na unyevunyevu kwenye ukingo wa msitu wa mvua ambapo wanakabiliwa na kibarua kizito cha kunusuru makubaliano ya mazingira duniani kutovunjika. Akifungua mkutano huo wa kimataifa, Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, alisema kuwa "mabadiliko ya tabia nchi sio tena kitisho cha baadae bali ni janga la wakati huu."

Lula aliwashutumu wale wanaokataa ushahidi wa kisayansi na "kueneza hofu, kushambulia taasisi, sayansi na vyuo vikuu," akiongeza kuwa ni nafuu sana kupigana kulinda mazingira kuliko kupigana vita. Amesema mkutano wa COP30 utakuwa wa kuambiana ukweli, katika enzi iliyotawaliwa na habari za uwongo na zisizo za kweli.

"Ongezeko la joto duniani linaweza kusukuma mamilioni ya watu kwenye njaa na umaskini, na hivyo kuondosha miongo kadhaa ya maendeleo. Athari zisizo na uwiano za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wanawake, watu wenye asili ya Kiafrika, wahamiaji na makundi yaliyo hatarini lazima izingatiwe katika sera za kukabiliana na hali hiyo. Ni muhimu kutambua jukumu la maeneo ya watu wa asili  na jumuiya za kitamaduni katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo," alisema Rais Lula.

Mkuu wa Mkutano wa UN kuhusu mazingira Simon StiellPicha: Pablo Porciuncula/AFP

Mazungumzo hayo yanafanyika bila uwepo wa Marekani, nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa mafuta duniani na pia mzalishaji wa pili wa gesi chafu, huku Rais Donald Trump ambaye mara kadhaa ametilia mashaka masuala yamabadiliko ya Tabianchi akitetea sekta ya mafuta na kukejeli nishati mbadala.

Wajumbe pia watalazimika kukabiliana na changamoto ya kushindwa kwa ulimwengu kufikia lengo la kihistoria la Mkataba wa Paris la kupunguza ongezeko la joto hadi 1.5C, baada ya wanasayansi na Umoja wa Mataifa kuonya katika siku za hivi karibuni kwamba kuvuka kiwango hicho kwa muda sasa ni jambo lisiloepukika.

Mkutano huo unafunguliwa katikati mwa dhoruba kali katika kanda ya Karibiani na Asia iliyoleta uharibifu mkubwa na hofu inayoongezeka kwamba mivutano ya kikanda kuanzia vita hadi uhasama wa kibiashara, vinazuia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Mkuu wa Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa Simon Stiell, alisifu maendeleo yaliyopatikana hadi sasa katika kupambana na ongezeko la joto duniani, lakini pia akionya juu ya udharura unaohitajika.

Bango la mkutano wa COP30 huko mjini Belem BrazilPicha: Mauro Pimentel/AFP/Getty Images

Stiell ameeleza hadhara ya COP30 kwamba Mkataba wa Mazingira wa Paris, uliohitimishwa miaka 10 iliyopita, umechangia kupungua kwa uzalishaji wa gesi chafu zinazoharibu hali ya hewa.

Mataifa tajiri na nchi zinazoendelea mara kwa mara huzozana katika mikutano ya COP kuhusu suala la ufadhili wa fedha zinazohitajika kwa mataifa maskini zaidi, ambayo yanachangia kidogo sana katika uchafuzi wa sayari, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kipindi cha mpito kutoka matumizi ya nishati ya mafuta.

Wakati huo pia kumetolewa utafiti leo ukionyesha kuwa uzalishaji wa gesi chafu nchini China ulipungua kwa kiasi katika robo ya tatu ya mwaka lakini uzalishaji wa nishati inayotokana na jua umeongezeka na matumizi ya magari ya umeme pia yanaendelea kukua.

Mnamo mwezi Septemba serikali ya China iliahidi kukomesha uzalishaji wa kaboni ifikapo mwaka 2030 na itakapofika mwaka 2035, itapunguza kati ya 7% hadi 10% kutoka kilele ambacho bado hakijajulikana.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW