Tsipras kuwasilisha mapendekezo
7 Julai 2015Wakati uchumi wa Ugiriki ukisuasua, na mabenki yakikaribia kufungwa siku ya Alhamisi kutokana na wasiwasi wa ukosefu wa fedha kwenye mashine za kutolea pesa, Ujerumani na Ufaransa zimeitaka serikali ya Tsipras kuwasilisha mapendekezo madhubuti katika jitihada za kujaribu kuyafufua tena mazungumzo ya kuusaidia uchumi wa nchi hiyo.
Baada ya kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema mlango wa mazungumzo uko wazi.
''Mlango bado uko wazi kwa mazungumzo, lakini ni muhimu sasa kwa Waziri Mkuu Tsipras kutoa mapendekezo madhubuti na ya kuaminika ili utayari wa kubakia kwenye kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro utafsiriwe kama mpango wa kudumu,'' alisema Hollande.
Mazungumzo ya viongozi hao yalifanyika hapo jana, siku moja baada ya Wagiriki kuyakataa masharti magumu yaliyopendekezwa na wakopeshaji wa kimataifa katika kura ya maoni ya kihistoria. Matokeo ya kura hiyo ni ushindi mkubwa wa kisiasa kwa Tsipras, lakini umeitumbukiza Ulaya kwenye mzozo.
Kwa upande wake, Kansela Merkel amesema masharti mapya kwa ajili ya kuuokoa uchumi wa Ugiriki bado hayajafikiwa na ndiyo maana wanasubiri mapendekezo sahihi kutoka kwa Tsipras, mpango ambao utairuhusu Ugiriki kurejea kwenye mafanikio. Amesema kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro tayari yameonyesha mshikamano mkubwa kwa Ugiriki.
Muda unayoyoma
''Muda unakimbia, hivyo mapendekezo kama hayo yanapaswa kuwasilishwa haraka wiki hii, ili tuweze kuutatua mzozo uliopo,'' alisisitiza Merkel.
Naye Kamishna wa Uchumi wa Kidigitali wa Umoja wa Ulaya, Gunther Oettinger ameviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kwamba bila ya kuwa na mapendekezo yoyote, mazungumzo yoyote yale mapya yatakuwa hayana maana.
Aidha, Waziri mpya wa Fedha wa Ugiriki, Euclid Tsakalotos amesema nchi yake ingependa kuendelea na mazungumzo na wakopeshaji wake. Tsakalotos aliteuliwa jana kushika nafasi ya Yanis Varoufakis aliyejiuzulu wadhifa huo mapema jana asubuhi.
Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker leo amesema hangependa kuiona Ugiriki inajiondoa kwenye kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro. Akizungumza katika Bunge la Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Ugiriki ilipopiga kura yake ya maoni kuyakataa mapendekezo ya wakopeshaji wa kimataifa, Juncker amesema hakuna mtu yeyote anayepaswa kufikiria kuiondoa Ugiriki kwenye kanda hiyo.
Ikulu ya Marekani imezitaka pande zote kutafuta muafaka utakaosaidia kuifanya Ugiriki kuurejea katika njia itakayofanikisha nchi hiyo kukua kiuchumi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman