1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 kwaajili ya Maendeleo ya Afrika magazetini

Oumilkheir Hamidou
16 Juni 2017

Mada kuuya Afrika magazetini wiki hii inahusiana na mkakati wa Ujerumani kwa Afrika , ingawa Kenya pia imezungumziwa kufuatia warsha ya GIZ iliyowasaidia wakulima kuimarisha mapato yao licha ya mabadiliko ya tabianchi

Deutschland G20 Afrika Treffen
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

 

Mada kuu iliyohodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii inahusiana na mkakati wa Ujerumani kwa Afrika , mkakati uliofafanuliwa mjini Berlin katika mkutano wa siku mbili wa mataifa 20 yaliyoendelea na yale yanayoinukia kiuchumi-G 20 kuhusu namna ya kuhimiza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Mada nyengine iliyochamabuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani itatufikisha Kenya ambako warsha iliyosimamiwa na shirika la Ujerumani la Ushirikiano wa kimataifa GIZ inasemekana imewasaidia watu kujizidishia mapato yao, kwa kuinua kilimo cha embe na viazi vitamu licha ya mabadiliko ya tabia nchi.

Tunaanza na mkutano wa G-20 kuhusu Afrika uliofanyika jumatatu na jumanne iliyopita mjini Berlin."Mkakati wa Ujerumani kwa Afrika ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Frankfurter Allgemeine linalozungumzia jinsi mpango wa maendeleo Marshall Plan  kwa Afrika, uliyogeuzwa jina na rais wa Niger Mahamadou Issoufou na kuitwa "Merkel Plan."Akihojiwa na gazeti hilo la mjini Frankfurt, rais wa Niger, alisema "ukitaka ufanisi wa kudumu, unahitaji mpango wa maendeleo". Rais Mahamadou Issoufou amemsifu kansela Merkel kwa kuelewa hali namna ilivyo barani Afrika; kwamba maendeleo, usalama na utawala bora pamoja pia na sera madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, haviwezi kutenganishwa. Na kansela pia anamwangalia rais wa Niger kuwa ni mmojawapo wa viongozi kadhaa wa Afrika wanaoweza kutegemewa."

 Frankfurter Allgemeine linazungumzia pia mikakati kadhaa iliyobuniwa na Ujeruani kwaajili ya bara la Afrika; Mbali na mkakati wa Marshall Plan uliopendekezwa na nwaziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller, kuna ule wa "Compact with Africa ulioandaliwa pamoja na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble. Lengo ni kubuni ushirikiano pamoja na mataifa ya Afrika ili kuimarisha taasisi za serikali na kubuni miradi ya kiuchumi kwa msaada wa hali na mali kutoka Ujerumani. Waziri Schäuble ameutaja mkakati huo utakaowarahisishia njia wawekezaji wa kibinafsi kuwekeza barani Afrika kuwa "mbinu ya aina mpya ya ushirikiano wa kiuchumi.

Frankfurter Allgemeine imeutaja pia mkakati ulioanzishwa tangu Frank Walter Steinmeier alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kwa jina "Mwongozo wa serikali kuu kuelekea Afrika."

Mkakati mpya kwa Afrika wawekewa suala la kuuliza

Berliner Zeitung limeuchambua pia mkutano huo wa siku mbili wa G20 kuhusu Afrika. Lakini kwa jicho la wasi wasi. "Demokrasia? Sio muhimu" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalojikita zaidi katika kuteuliwa mataifa mfano Misri, Ethiopia na Rwanda kushiriki katika mkutano huo." Ni dhahir kwamba lengo hapo sio kuhimiza demokrasia na kuhakikisha misaada inawafikia wale wanaoihitaji. Kinachotakiwa zaidi hapa ni maeneo ya uwekezaji yatakayozipatia natija  kubwa kubwa nchin za viwanda. Berliner Zeitung linasema hakuna anaebisha umuhimu wa vitega uchumi kwa Afrika lakini muhimu ni kujua wapi na kwa masharti gani.

Warsha ya shirika la Ujerumani la Ushirikiano wa kimataifa GIZ nchini Kenya

"Faida ya Misaada" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Berlin Der Tagesspiegel kuhusu mradi uliosimamiwa na shirika la Ujerumani la ushirikiano wa kimataifa GIZ nchini Kenya. Katika warsha iliyosimamiwa na shirika hilo wakenya wamejifunza jinsi la kupandisha miembe mingi zaidi na viazi itamu, licha ya mabadiliko ya tabia nchi. Mafunzo hayo yamewawezesha kuzidisha kipato chao, linaandika gazeti la der Tagesspiegel linalotoaa mfano wa Charles Ogolla na mkewe Eveline wanaoishi umbali wa kilomita 300 kutoka mji mkuu Nairobi. Charles Ogolla alikuwa kabla ya hapo akifanya kazi ya ulinzi, ambayo anasema mshahara haukuwa mzuri na masharti ya kazi pia hayakuwa mazuri. Alipochoshwa na hali hiyo akaamua miaka kumi iliyopita kurejea katika kijiji alikozaliwa Kakamega ambako wazee wake wanamiliki ekari nne  za ardhi. Kilichompa moyo kufanya hivyo ni mafunzo aliyoyapata kupitia shirika la Ujerumani la GIZ, linaandika der Tagesspiegel linalokumbusha asili mia 70 ya wakenya milioni 48 wanategemea kilimo na asili mia 30 ya pato la ndani la Kenya linatokana na sekta ya kilimo.

.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL PRESSE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

.