Mkutano wa G20 umemalizika
12 Novemba 2010Viongozi wa nchi za kundi la G20 leo wameidhinisha sheria kali za kusimamia Taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria zitakazoangalia viwango vya pesa katika Mabenki ili kuzuia hatari ya kutokea tena mporomoko wa kiuchumi duniani.
Viongozi hao wa kundi la G20 wamekamilisha mkutano wao wa kilele mjini Seoul hivi punde kwa kupitisha azimio linalounga mkono hatua za kuboresha taasisi kubwa za fedha duniani,ambazo zimekuwa zikionekana haziwezi kupata matatizo ya kiuchumi.
Katika taarifa ya viongozi hao wamesema kwamba mpango mpya uliokubaliwa utahakikisha kwamba mfumo wa fedha unadhibitiwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni kwa lengo la kuimarisha uchumi wa dunia.
Wakuu hao wa nchi tajiri wamejadiliana katika kikao cha siku mbili kuhusu kisomo walichokipata kutokana na mporomoko wa masoko ya fedha duniani ulioshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni, ambapo pia wamezungumzia suala la kuwepo haja ya kupunguza kitisho cha kuanguka kwa mabenki makubwa duniani na kusababisha mtikisiko wa kiuchumi.
Wamekiri katika kikao hicho kwamba ulimwengu umejifunza kisomo kikubwa baada ya kuporomoka kwa benki ya Lehman Brothers ya Marekani mwaka 2008, hali iliyosababisha mshutuko mkubwa wa kiuchumi kote duniani. Akizungumza hivi punde rais Obama amesema.
''Tulikuja Seoul kuendeleza kazi iliyotupeleka kuanzia London, Pittsburg hadi Toronto.Tuatashirikiana kuukwamua uchumi wa dunia kutoka kwenye janga kubwa.Tunataka kuepuka mporomoko wa masoko ya fedha kulikosababisha kuanguka kwa uchumi wa dunia. Tumeamua kuzingatia mizani sawa katika kuukuza na kuuendeleza uchumi. Pia tumekubaliana juu ya mpango wa kuchukua hatua katika kukabiliana na rushwa''
Viongozi wa G20 wamesema kwamba hatua hiyo ya kuyadhibiti mabenki na taasisi za fedha imetokana na hali iliyoshuhudiwa mwaka 2008 ya kutowajibika kwa viongozi wa vyombo hivyo pamoja na kuwepo dosari kubwa katika sheria na usimamizi wa Mabenki hayo.
Ama kwa upande mwingine, nchi zenye nguvu katika Umoja wa Ulaya, Uingereza Ufaransa, Ujerumani, Itali na Spain zimetoa taarifa ya pamoja katika mkutano huo wa Seuol zikisisitiza kwamba mpango mwingine wa kuupiga jeki uchumi unaweza tu kufanyika katikati ya mwaka 2013 bila ya kuathiri mipango ya wakati huu.
Aidha Kansela Merkel amezungumzia pia wasiwasi uliopo kuhusiana na ati ati za Ireland kujikuta katika mporomoko wa kiuchumi. Amesema walipa Kodi wa nchi za Ulaya hawapaswi kubeba mzigo wa kulipia gharama zote za kuziokoa nchi zinazozongwa na madeni. Lakini kwa mujibu wa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, Umoja huo umejiandaa kuisaidia mkono Ireland.
Mkutano mwingine wa G20 umepangwa kufanyika Ufaransa mwakani ambapo tayari rais Nicolas Sarkozy ameshawaalika viongozi wa kundi hilo katika mji wa Cannes.
Mwandishi Saumu Mwasimba/APE
Mhariri Othman Miraji