Mkutano wa G20 waanza Canada
27 Juni 2010TORONTO
Viongozi wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi- G-20 wameanza mkutano wao wa kilele mjini Toronto. Viongozi hao wa mataifa hayo 20 walilakiwa na mwenyeji wao Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper. Canada pia ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliomalizika kwa kundi la nchi nane tajiri duniani- G-8. Katika mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao watajadili mkakati wa kuongeza nguvu harakati za kufufua uchumi pamoja na mpango tata wa kuyadhibiti masoko ya fedha. Kundi hilo la G-20 ni kundi jipya, ambalo mkutano wake wa kwanza ulifanyika mjini Pittsburg, Pennsylvania na linayaleta pamoja mataifa manane tajiri duniani, pamoja na nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile Australia, Brazil, China na India. Nchi nane tajiri kiviwanda, Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Itali, Urusi na Marekani zilimaliza mkutano wao wa siku mbili jana, kwa kuahidi dola bilioni 7.3 katika miaka mitano ijayo, kupambana na vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Mkutano huo pia uligusia masuala ya usalama, ikiwemo Iran, Korea Kaskazini, Afghanistan, Pakistan na Mashariki ya Kati.