1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7 Japan

John Juma26 Mei 2016

Rais Obama anayehudhuria mkutano huo anatarajiwa kufanya ziara ya kihistoria ya kuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzuru eneo la Hiroshima ambalo Marekani ilifanya shambulizi la kwanza kwa bomu la atomiki nchini Japan.

Viongozi wa G7 wakiwa Ise-Shima.
Viongozi wa G7 wakiwa Ise-Shima.Picha: Getty Images/AFP/S. De Sakutin

Viongozi wa mataifa saba tajiri duniani kiviwanda wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya uchumi duniani. Viongozi hao wamekubaliana na wito uliotolewa wa kugharamia kwa njia inayofaa kuimarisha uchumi wa dunia. Lakini kila taifa litaamua kivyake kiwango cha fedha na ni wakati gani kutimiza makubaliano hayo. Hayo yamesemwa na Naibu katibu wa baraza la mawaziri Japan Hiroshige Seko ambaye pia ameongeza kuwa wanachama wengine hawakuona sababu ya kutumia fedha zaidi.

Viongozi wa kundi la G7 wameanza mkutano wao mjini Ise-Shima nchini Japan kwa kuelezea changamoto zinazozikabili nchi ambazo uchumi wao unakua. Hata hivyo kuliibuka kauli kinzani kuwa hali iliyopo si ya mzozo. Uingereza na Ujerumani zimekuwa zikipinga wito unaounga mkono mkakati wa kifedha kukabiliana na changamoto za kiuchumi duniani. Naibu katibu wa baraza la mawaziri nchini Japan Hiroshige Seko amewaambia waandishi habari.

kushuka kwa bei ya bidhaa

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alionyesha takwimu jinsi bei ya bidhaa ulimwenguni zilivyoshuka kwa asilimia 55 tangu Januari mwaka 2014 hadi Januari 2016, kiwango sawa na kati ya Julai mwaka 2008 na Februari 2009 baada ya kuporomoka kwa benki iliyosifika Marekani Lehman Brothers. Rais wa Marekani Barrack Obama amethibitisha kuwa"wamezungumzia masuala kadha wa kadha yakiwemo uchumi wa dunia na haja ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, mazungumzo ya kibiashara. Pia tumegusia masuala ya usalama na tunajadili zaidi katika awamu ijayo ya mjadala."

Rais Barack Obama na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe.Picha: Reuters/T. Hanai

Viongozi wa G7 pia wanatarajiwa kusisitiza uamuzi wao wa awali wa udhibiti wa soko la fedha za kigeni. Awali rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk alisema atatafuta uungwaji mkono wa viongozi wa kundi h ilo kuitisha msaada zaidi kwa wakimbizi. Idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Syria na kwingineko kuelekea Ulaya imesababisha changamoto kubwa ambayo haijawahi kulikumba bara la Ulaya tangu vita vikuu vya pili duniani "Tusipoongoza katika kudhibiti mzozo huu, hakuna atakaye fanya" Tusk amesema.

Mada nyinginezo za kujadiliwa katika mkutano huo ni jinsi ya kushirikiana na kuimarisha vita dhidi ya ugaidi, usalama wa mitandao na usalama wa baharini hasa mvutano wa umiliki wa sehemu za bahari kati ya china na Japan na mataifa mengine ya bara Asia.

Obama kuzuru Hiroshima

Rais Obama anayehudhuria mkutano huo anatarajiwa kufanya ziara ya kihistoria kama rais wa kwanza wa Marekani kuzuru eneo la Hiroshima ambako Marekani ilifanya shambulizi la kwanza la bomu la atomiki wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia mwaka 1945.

Ziara ya Obama katika bustani ya amani ya Hiroshima inahofiwa itapata umaarufu zaidi na hata kuumeza mkutano wenyewe. Hata hivyo baadhi ya wajapan wametaka Marekani kuondoa majeshi yake nchini humo hasa kufuatia kisa cha mfanyakazi wa kambi ya jeshi la Marekani kushikwa kwa kuhusishwa na mauaji ya mwanamke mmoja raia wa japan katika kisiwa cha Okinawa.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anahudhuria mkutano huo huku suala la nchi yake kupiga kura ya maamuzi mwezi ujao kujitenga au kusalia katika Umoja wa Ulaya likitarajiwa kujipenyeza kwenye mkutano huo.

Viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Ufaransa Francoise Hollande, kiongozi wa Italia Matteo Renzi na wa Canada Justin Trudeau.

Maafisa wa Japan wamesema wameimarisha usalama huku maelfu ya polisi wakishika doria katika maeneo na vituo mbalimbali.

Mwandishi: John Juma/RTRE/

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW