Mkutano wa G7 kujadili uchumi unaozorota
9 Septemba 2011Ufaransa, iliyo mwenyeji wa mkutano huo wa G7, imetoa mwito kuchukua hatua zilizoratibiwa na mataifa hayo tajiri, baada ya wasiwasi kuzuka kwa sababu ya mzozo wa madeni barani Ulaya na kusababisha thamani ya hisa kuporomoka vibaya katika masoko ya fedha hivi karibuni. Lakini matatizo tofauti ya kiuchumi yanayokabiliwa na Marekani, Uingereza na nchi za kanda inayotumia sarafu ya Euro, hutatanisha kazi hiyo. Hakuna ufumbuzi mmoja kwa matatizo yanayotofautiana.
Taarifa kutoka mjini Brussels Ubeligiji inasema, mkutano wa G7 huenda ukakubaliana sera ya kuendelea kuweka kiwango kidogo cha riba, kupunguza nakisi na madeni ya serikali, kule kunakowezekana na kufanya mageuzi katika mfumo wa uchumi. Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Francois Baroin amesema, kila nchi katika kundi hilo la G7 ichukue hatua kuambatana na hali yake ya kiuchumi. Hapo awali, Waziri wa Fedha wa Marekani, Timothy Geithner alisisitiza kuwa ni lazima kuchukua hatua za kusaidia ukuaji wa kiuchumi.
Kwa mujibu wa tathmini ya shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD, ukuaji wa kiuchumi katika nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda, utapungua katika robo ya mwisho ya mwaka huu, ukilinganishwa na ukuaji wa miezi mitatu iliyopita. OECD imetoa mwito kwa viongozi wa G7 na magavana wa benki kuu, kuchukua hatua za kuchangamsha uchumi unaozorota .Benki Kuu zimehimizwa kuendelea na kiwango cha chini cha riba na kuzingatia hatua zingine za kusaidia ukuaji wa kiuchumi.
Japan inatazamiwa kuujadili mzozo wa madeni unaoakabiliwa na nchi za kanda inayotumia sarafu ya Euro barani Ulaya, wakati nchi za Asia zikiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mzozo huo wa madeni katika nchi za magharibi pamoja na ukuaji wa kiuchumi unaozorota. Japan huenda ikaeleza wasiwasi wake kuhusu uimara wa sarafu yake Yen na ikajiamulia kuchukua hatua ya upande mmoja. Mkutano wa G7 nchini Ufaransa, umepewa umuhimu maalum kwa sababu ya hofu kuwa uchumi hivi sasa huenda unapitia kipindi kigumu kabisa, tangu ulipotokea mzozo wa fedha mwaka 2008 kote duniani.
Mwandishi: Martin,Prema/rtre
Mhariri:Mwadzaya, Thelma