1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani yakutana

Abdu Mtullya7 Juni 2015

Viongozi wa mataifa makuu saba ya kiuchumi duniani wanaanza mkutano wa kilele wa siku mbili katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani ambao pia unahudhuriwa na viongozi kadhaa wa nchi za Afrika kama waalikwa.

Viongozi wa mataifa saba yenye nguvu za kiuchumi duniani wakiwasili kwenye moja ya mikutano yao ya kilele.
Viongozi wa mataifa saba yenye nguvu za kiuchumi duniani wakiwasili kwenye moja ya mikutano yao ya kilele.Picha: Getty Images/AFP/A. Jocard

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani leo atawalaki viongozi wenzake wa mataifa hayo makuu saba ya kiuchumi duniani watakaoshiriki kwenye mkutano wa kundi la nchi linalojulikana kama G7.

Kwenye mkutano wao huo, viongozi wakuu wa nchi hiyo watazungumzia juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, mgogoro wa Ukraine, ugaidi, biashara, uchumi na juhudi za kupambana na maradhi ya milipuko. Pia wataujadili mgogoro wa madeni wa Ugiriki.

Merkel kusisitiza umuhimu wa mazingira

Akiwa mwenyeji wa mkutano huo wa kilele, Kansela Merkel anatarajiwa kuitumia fursa ya mkutano huo kuwashawishi viongozi wengine kuhusu umuhimu wa kuyaunga mkono makubaliano juu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa pamoja na kuwataka watoe ahadi ya kuweka kikomo katika ongezeko la joto duniani cha nyuzi joto 2 kwa kipimo cha Celsius, kwa mujibu wa mwito uliotolewa na wataalamu wa mambo ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa.

Kuupata msimamo thabiti wa nchi hizo 7 tajiri ni muhimu kwa ajili ya mazungumzo juu ya suala la mabadiliko ya hali ya hewa yatakayofanyika mjini Paris mnamo mwezi wa Desemba, ambapo nchi zaidi ya 190 zitajaribu kuupitisha mkataba wa kuziwajibisha nchi zote, ili uanze kutekelezwa mnamo mwaka wa 2020.

Polisi wakilinda eneo la mkutano nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/K.-J. Hildenbrand

Mgororo wa Ukraine kujadiliwa

Suala jingine litakalozingatiwa kwenye mkutano huo wa viongozi wa nchi saba tajiri ni mgogoro wa nchini Ukraine.

Kansela Merkel kwa mara nyingine anatarajiwa kuyapinga maombi ya Ukraine na shinikizo la wabunge wa Marekani juu ya kuipatia Ukraine silaha kutoka Marekani ili iweze kuyaimarisha mashambulizi ya majeshi yake dhidi ya waasi wa mashariki wanaoungwa mkono na Urusi.

Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kuwaomba viongozi wa Ulaya wakubali kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

Ukraine na nchi za magharibi zinamlaumu Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa kuchochea mvutano na kwa kuwaunga mkono kijeshi waasi wanaotaka kujitenga.

Mwenyeji wa mkutano wa kilele wa G7, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mwaka uliopita Urusi iliondolewa kwenye kundi hilo ambalo hapo awali lilikuwa la nchi nane, G8, kwa sababu ya hatua iliyochukua ya kuliteka jimbo la Krimea ambalo ni sehemu ya Ukraine.

Mjadala juu ya ugaidi

Viongozi kutoka Iraq, Tunisia na Nigeria wamealikwa kwenye mkutano huo wa mataifa makuu saba ya viwanda, ambapo watashiriki katika kuijadili hatari inayotokana na magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu.

Kuhusu biashara, viongozi wa nchi za Ulaya waliomo katika kundi la G7 wanakusudia kupiga hatua kwenye mazungumzo juu ya masuala ya biashara na wenzao wa Marekani, Japan na Canada. Mjadala mkali wa kisiasa unahusu pendekezo juu ya ubia wa kibiashara na uwekezaji vitega uchumi baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya.

Pendekezo hilo linakabiliwa na upinzani mkali nchini Marekani na barani Ulaya kutoka kwa watu wenye wasiwasi juu ya athari za ubia huo katika sekta za ajira, mazingira na usalama wa vyakula na bidhaa.

Vikatuni vya viongozi wa G7 kutoka kwa waandamanaji wanaolipinga kundi hilo la mataifa tajiri.Picha: Reuters/M. Rehle

Viongozi wa nchi saba tajiri pia watauzungumzia mgogoro wa madeni wa Ugiriki.

Maandamano ya wanaharakati

Hata hivyo, mkutano wa viongozi hao unakabiliwa na upinzani mkubwa hasa wa vijana, ambapo watu wapatao 3,000 walifanya maandamano jana ya kuupinga, lakini polisi 17,000 waliwekwa tayari kuwakabili waandamanaji hao. Polisi wengine 2,000 wa Austria pia wamewekwa tayari karibu na mpakani.

Mkutano huo unaofanyika katika mji wa Elmau katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani unahudhuriwa na viongozi kutoka Ujerumani, Marekani, Japan, Uingereza, Ufaransa, Italia na Canada.

Mwandishi: Mtullya Abdu/ape,dpa
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW