Mkutano wa G8 kuanza leo nchini Italia.
8 Julai 2009Rais wa Marekani Barack Obama amewasili nchini Italia hii leo kuhudhuria mkutano wa nchi tajiri kiviwanda duniani za G8. Rais Obama anayetokea mjini Moscow nchini Urusi, anatarajiwa kukutana na rais wa Italia Giorgio Napolitano kabla ya kuelekea katika mji wa L`Aquila kunakofanyika mkutano huo.
Viongozi hao wa nchi nane tajiri duniani za G8, wanakutana kwa lengo la kuukabili kwa pamoja mzozo wa kiuchumi unaoikumba dunia hivi sasa, lakini hata hivyo wanatofautiana kuhusu ni muda gani wataendelea kuufufua uchumi.
Viongozi wa Uingereza , Canada, Ufaransa , Ujerumani , Italia, Japan , Urusi na Marekani wote wanatarajiwa kukusanyika katika mkutano huo. Huku viongozi hao wakiendelea kuwasili nchini Italia, zaidi ya wanaharakati 100 wanaopinga uchafuzi wa mazingira kmutoka kote duniani walikusanyika katika vituo vya kawi vinayotua makaa ya moto kote nchini Italia, wakitaka viongozi hao kulitilia maanani suala la mabadiliko ya hali ya hewa.
Rais wa China Hu Jintao hatahudhuria mkutano huo kufuatia ghasia zinozoendelea kaskazini magharibi mwa China ambapo watu 156 wameuawa. Kutokuwepo kwa rais Jintao huenda kukatatiza juhudi za kuafikia makubaliano ya kupunguza kupanda kwa joto duniani.
Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi anayekabiliwa na kashfa za kimapenzi ataufungua rasmi mkutano huo ambao kwanza utazungunzia suala la uchumi duniani. Maafisa kutoka ulaya wanasema kuwa viongozi hao wanatarajiwa kukubaliana kuwa uchumi wa dunia uko katika hali mbaya na hatua zaidi zinahitajika.
Akiongea na waandishi wa habari waziri mkuu wa uingereza Gordon Brown alisema kuwa ulimwengu unastahili kuliweka mbele suala la kuufufua upya uchumi. Matamshi yake yanatarajiwa kuungwa mkono na Marekani,Japan na Ufaransa na kuiacha nje Ujerumani nchi iliyo na uchumi dhabiti zaidi barani ulaya ambayo inasema kuwa ni bora nchi za G8 kuacha kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa makampuni yanayokabiliwa na hatari ya kusambaratika wakati uchumi utakapo imarika.
Viongozi wa G8 hawakulitilia maanani tatizo la mzozo wa kuichumi lililo kuwa likizikabili nchi zao walipokutana nchini Japan mwaka uliopita na mkutano wa eleo utazungumzia hatua zinazostahili kuchukuliwa ili kuzuia hali kama hiyo kutokea tena.
Hata hivyo maafisa wanasema kuwa matumaini zaidi yalitarajiwa katika mkutano wa nchi tajiri duniani za zile zinazoinukia kiuchumi za G20 ulioandaliwa mjini London mwezi Aprili mwaka huu na ambao pia unatarajiwa kuandaliwa nchini Marekani mwezi Septemba mwaka huu.
Rias wa china Hu Jintao alitarajiwa kutumia mkutano huo kuziambia nchi zingine kuwa, kunastahili kuwa na sarafu nyingine kama sarafu ya dola.
Kwa upande mwingine ujumbe kutoka china ambao utahudhuria mkutano huo huku waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi akisema kuwa amekabilwa na pingamizi kutoka china kuhusiana na juhudi zinazofanywa na mataifa ya G8 za kuondoa tofauti juu ya gesi inayochafua mazingira na kufadhili teknolojia isiyochafua mazingira.
Viongozi hao wa G8 pia wanatarajiwa kuzungumzia pendekezo la Marekani kuwa nchi tajiri zinastahili kutoa msaada ya dola biloni 15 kwa nchi maskini utakao tumika katika maendeleo ya kilimo huku marekani ikisema kuwa iko tayari kutoa msaada wake wa kati ya dola bilioni na tatu na nne.
Mwandishi : Jason Nyakundi/RTRE
Mhariri : Othman Miraji