Mkutano wa hali ya hewa Copenhagen
1 Desemba 2009Mkutano ujao mjini Copenhagen,Denmark, kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, utaathiri mustakbala wetu ama kwa njia nzuri au mbaya:
Swali linalozuka , ni kwa kadiri gani, mkutano huo umejizatiti kupambana barabara na mabadiliko hayo ya hali ya hewa ? Kwani, sio tu ni swali la badiliko la hali ya hewa bali pia kuna mambo mengine yanayochangia kupunguza moshi unaopaa hewani na kuchafua hewa.
"Naamini kwamba, mkutano wa Copenhagen, utaleta mabadiliko zaidi na kuwezesha pia kuchangiwa pia fedha zaidi.Ni mabadiliko ambayo hata bila ya mkutano huo wa Copenhagen yangetokea."
Alisema Yvo de Boer, Kiongozi wa Halmashauri ya Uandishi ya Umoja wa Mataifa kwa maswali ya hali ya hewa.Kwa jinsi aonavyo yeye, hakuna shaka kuwa, dunia sasa inalikabili tatizo hili la mabadiliko ya hali ya hewa ,bali swali ni kwa kasi gani na jitihada gani .Bila shaka, akiwa mjumbe mkuu wa UM anaetetea mazingira safi ,anaona haja kubwa iliopo kukubaliana Copenhagen, kanuni za kuwajibika mataifa yote .Kwani hata bila kuwapo kanuni hizo ,ulimwengu hauwezi kuepuka kufuata mkondo wa kuepukana na dhara za uchafuzi wa hali ya hewa.
Yvo de Boer anaongeza:
"Kuna wakati najiuliza: ingekuaje laiti , majadiliano kama hayo yangefanyika miaka 50 iliopita.Wakati ule, wanadamu wakisema :La, haiwezekani kabisa ifikapo mwaka 2009, tutakua na ndege za kusafiria na zana za usafi majumbani mwetu.Jinsi gharama zake zilivyo kubwa , vyombo kama hivyo, havitakuwapo.Naamini mabadiliko haya kwa njia hii au ile, yatatokea tu kwa sababu, mkondo huu wa leo, hautokani tu na mabadiliko ya hali ya hewa...."
Mjumbe huyo wa UM anasema zaidi kwamba, mabadiliko ya hali ya hewa, ni swali muhimu zaidi, lakini tunazungumzia pia kupanda kwa bei ya mafuta,usalama wa nishati kwa jumla na uzuri wa hewa tunayovuta.Ufundi na teknolojia nyingi tunazotumia leo, anasema de Boer, zimepitwa na wakati.
Mabadiliko ya kuwa na dunia bila moshi unaochafua mazingira , hayataamuliwa pekee na mkutano juu ya uchafuzi wa hali ya hewa.Hivyo, ndivyo asemavyo Bw.Rainer Wend, Kiongozi wa Idara maalumu katika kampuni la DHL,shirika kubwa la mipango ya huduma za mipango,uchukuzi na mawasiliano.
Anasema kwamba, katika kampeni lao, wanalenga ifikapo 2020, kuzidisha kwa 30% ubora wa kazi zao ili kupunguza mivuke inayochafua hali ya hewa .Na hiyo, anasema, ni shabaha kubwa kuifikia ,lakini wanajitahidi.
Pili, anaongeza, Wend, kampuni lake linataka kutengeneza bidhaa na zana zisizochafua hali ya hewa kwa moshi unaopaa hewani. Hii ina maana ,wateja ama wa kibinafsi au wanabiashara, wataweza kupewa huduma na kampuni la DHL za kutuma barua au bahasha zao kwa njia ambazo hazichafui hali ya hewa.
Mtayarishi: Ramadhan Ali
Uhariri: Abdul-Rahman