Viongozi wa India na Afrika wajadili ushirikiano wa biashara na uchumi
8 Aprili 2008
Mkutano wa kihistoria wa viongozi wa India na nchi za Afrika umeanza leo mjini New Delhi kujadili njia za kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kibalozi baina ya mabara yao.
Viongozi wasiopungua 15 kutoka nchi za Afrika wanahuhduria mkutano huo wa siku mbili ambapo pamoja na wenyeji wao wa India wanajadili njia za kuimarisha uhusiano wa kiabiashara na kiuchumi.
Mkutano huo ni muhimu kwa kutambua kwamba biashara baina ya India an nchi za Afrika sasa imefikia thamani ya dola bilion 30.
Biashara baina ya pande hizo imekuwa inaongezeka tokea mwaka 2001.
Kwenye mkutano wao viongozi wa India na Afrika pia watajadili ushirikiano katika sekta za nishati na usalama.
Mkutano huo unafanyika wakati ambapo India, nchi inayoinukia kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi inahitaji nishati na raslimali zaidi kwa ajili ya uchumi wake unaondelea kustawi kwa kiwango kikubwa.
Biashara baina ya India na nchi za Afrika imekuwa inastawi haraka mnamo miaka ya hivi karibuni na imeongezeka mara mbili.Pande mbili hizo zinakusudia kuongeza zaidi kiwango cha biashara baina yao ambacho sasa kinafikia thaamni ya dola bilioni 30.
Akifungua mkutano huo leo mjini New Delhi waziri mkuu wa India bwana Manmohan Singh amesema nchi yake inataka kuona karne hii kuwa ni ya watu wa Afrika na India wakishirikiana katika juhudi za kuendeleza sera za dunia utandawazi.
Waziri mkuu huyo pia ametangaza kupunguza ushuru kwa bidha za Afrika zinazouzwa nchini India Amesema India pia itashirikiana na nchi za Afrika katika sekta za kilimo,miundombinu,elimu ,pamoja na mawasiliano ya kisasa.
Na katika kipindi cha miaka mitano ijayo India itatoa mikopo thamani ya dola bilioni 5 na milioi mia nne.
Akizungumza kwenye mkutano huo rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo amesema katika ushirikiano wake na nchi zingine mnamo miaka ya nyuma Afrika iliambulia maneno matupu. Rais Kabila amesema Afrika sasa inataka kuona miradi ya haraka katika maendeleo.