1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Washirika wa NATO waahidi mshikamano zaidi na Ukraine

12 Julai 2024

Viongozi wa Jumuiya ya NATO wamekubaliana kuendelea kuiunga mkono Ukraine walipokuwa wakihitimisha mkutano wao wa kilele uliogubikwa na mashaka juu ya uwezo wa Rais Joe Biden wa kuwania tena urais nchini Marekani.

Marekani NATO-Mkutano wa kilele Washington |
Viongozi wa mataifa ya jumuiya ya kujihami, NATO katika maadhimisho ya miaka 75 wamekubaliana kuendelea kuisaidia UkrainePicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Biden alitumia jukwaa hilo kujaribu kuwashawishi Wamarekani kwamba bado anaweza kuwaongoza. Kwenye NATO bado viongozi wenzake, wanamuamini, japo wakati mwingine kwa shakashaka. Kile wasichopenda kukishuhudia ni Donald Trump kurudi madarakani.

Hata kile cha kukosea majina wakati akiufunga mkutano huo, kama aliposema "Putin" badala ya "Zelensky" ama "Trump" badala ya "Kamala Harris", hakikuchukuliwa na viongozi wenzake kama tatizo. Wengine kama Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz walisema, "mtu yoyote anaweza kukosea." 

Muungano huo wa mataifa 32 ulitumia kusanyiko hilo wakati ukiadhimisha miaka 75, kuonyesha msimamo wao  dhidi ya Urusi, miaka miwili na nusu tangu Urusi ilipovamia Ukraine anayeungwa mkono na Magharibi. 

Kwenye mkutano na waandishi wa habari wa kuhitimisha mkutano huo, Biden alisisitiza kwamba kamwe hataigeuzia mgongo Ukraine na kuahidi kuendelea kuiimarisha NATO. 

Rais Joe Biden akipeana mkono na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine walipokutana kwa mazungumzo wakati wa mkutano wa kilele wa NATOPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Viongozi wa Jumuiya ya NATO walikubaliana kuendelea kuiunga mkono Ukraine walipokuwa wakihitimisha mkutano wa kilele wa siku tatu uliogubikwa na mashaka juu ya uwezo wa Rais Joe Biden wa kuwania tena urais nchini Marekani.

Muungano huo wa mataifa 32 ulitumia kusanyiko hilo wakati ukiadhimisha miaka 75, kuonyesha msimamo wao  dhidi ya Urusi, miaka miwili na nusu tangu ilipomvamia jirani yake Ukraine anayeungwa mkono na Magharibi. 

Washirika wa NATO hawakutoa mwaliko wa wazi kwa Ukraine kujiunga nao

Rais Volodymyr Zelensky aliwaomba washirika wa NATO na hasa Marekani kuendelea kuwasaidia na kuondoa vizuizi vya namna jeshi lake linavyoweza kutumia silaha wanazosaidiwa ili kushambulia ndani ya Urusi. 

Washirika muhimu wa Ukraine walilegeza masharti ya namna Ukraine inavyoweza kutumia silaha za msaada mnamo mwezi Mei na Rais Biden amesema jana kwamba bado anasikiliza ushauri kutoka kwa maafisa wake wa kijeshi na kutathmini ili kuona kama kuna haja ya kulegeza zaidi. 

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani(katikati) akiteta jambo na Rais Joe Biden na pembeni yao ni Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, Julai 10, 2024Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Kansela Scholz alikuwa wazi zaidi aliposema hakuna anayepanga kubadilisha hatua na miongozo iliyowekwa mwezi Mei na kuongeza kuwa bado wana jukumu ya kuendeleza wajibu wa kuisaidia ukraine kwa kiwango cha juu kabisa, na kwa upande mwingine kujaribu kwa kila namna kuzuia vita hivyo kutanuka. 

Soma pia:Zelensky atembelea Donetsk eneo la mstari wa mbele la vita

Viongozi kwenye mkutano huo walimvunja moyo Zelensky baada ya kukataa kutoa mwaliko wa wazi kwa Ukraine kujiunga na ushirika wa NATO, ingawa walipulizia makali hayo kwa kusema tu kwamba, hawatabadilika kimtazamno kuelekea ombi hilo la Ukraine.

Siku hiyo ya mwisho ya mkutano, iligubikwa na masuala ya uhusiano wa kimataifa, kuanzia kikao cha Baraza la NATO la masuala yahusuyo Ukraine hadi mazungumzo kati ya NATO na mataifa manne ya Kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki ya Japan, Korea Kusini, Australia na New Zealand.

Mazungumzo yao yalimalizika kwa tamko la pamoja la "kulaani vikali ushirikiano haramu wa kijeshi" kati ya Urusi na Korea Kaskazini, hatua inayoashiria namna NATO na mataifa hayo yanavyozidi kuimarisha ushirikiano wa kukabiliana na kile wanachokiona kama kitisho cha pamoja cha usalama.

Mkutano huu wa Washington ni wa tatu wa aina hiyo uliohudhuriwa na viongozi kutoka mataifa hayo manne washirika wa NATO.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW