Mkutano wa Jumuiya ya Madola wafanyika Sri Lanka
15 Novemba 2013Mkutano wa nchi za jumuiya ya madola, umeanza leo mjini Colombo, Sri Lanka. Wakati viongozi wa Canada, India na Mauritius wamegoma kushiriki kwa kile wanachodai nchi hiyo inapaswa kutengwa na shughuli za kijumuiya, kutokana na kitendo chake cha kutoruhusu upelelezi wa kimataifa kufanyika nchini humo kuhusiana na tuhuma za mauaji ya kivita, wakati nchini nyingine wanachama wanaona kuihusisha nchi hiyo ni moja ya mbinu ya kuiingiza katika mjadala wa hatua za kidemokrasia nchini humo.
Mkutano huo wa nchi za jumuiya ya madola umefunguliwa rasmi leo kwa hotuba ya rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa, ambaye katika hotuba hiyo, kulikuwa na maneno ya kumuomba Mungu wa imani ya watu wa taifa hilo yaani Budha, kwamba ayaadhibu mataifa yote yanayoituhumu nchi hiyo kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu na kutokuwepo kwa demokrasia.
Kwa nini mkutano ufanyike Sri Lanka?
Jumuiya ya madola imepingwa vikali na baadhi ya wanachama wake, kwa uamuzi wa kufanyia mkutano huo katika visiwa hivyo vya Sri Lanka kutokana na uongozi wa nchi hiyo kutokuwa tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa, iliyotaka kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji ya kivita yaliyotokea nchini humo, yaliyosababishwa na jeshi la nchi hiyo katika vita vilivyodumu kwa miaka 27.
Rais Mahinda wa Sri Lanka na kaka yake ambao wameshikilia madaraka katika nchi hiyo tangu mwaka 2005, ameng'anga'nia msimamo kuwa jeshi la nchi yake halijafanya vitendo vyovyote vya ukiukaji wa haki za binaadamu, ambapo katika hotuba yake alikuwa na maneno aliyoyanukuu kutoka katika imani yao ya budha yanayosema," usijali makosa yaliyofanywa na wengine, bali jali yale unayofanya mwenyewe" .
Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, alipanga ziara ya kwenda kutembelea eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, ambako ndiko kuna vita vinavyoendelea kati ya jeshi la nchi hiyo na wapinzani ambao ni watu wa kabila la Tamil, baada ya uzindizi wa mkutano huo mjini Colombo.
Cameron akiongea na kituo cha televisheni cha SKY news, alisema ni vyema Rajapaksa kukubali hali halisi inayodaiwa na umajo wa mataifa na Marekani, na hivyo aruhusu uchunguzi ufanyike nchini mwake.
Mpaka sasa mamia ya watu wa kabila la Tamil, walioathirika zaidi na vita nchini humo, wamefanya maandamano katika mji wa Jaffna kwenye eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, na waandamaji wengine walikuwa katika mji wa Colombo ambako ndiko unakofanyika mkutano huo, huku wakiwa na mabango makubwa, wakidai serikali iwajibu kuhusiana na vifo vya maelfu ya watu wa eneo hilo na maelezo ya kupotea kwa baadhi ya watu pasipo kujua walikopotelea, ambapo tuhuma zote hizo wanazielekeza kwa serikali yao.
Mwandishi:Diana Kago/AP
Mhariri:Josephat Charo