Mkutano wa jumuiya ya NATO waanza leo nchini Romania
2 Aprili 2008Mkutano wa kila mwaka wa jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi NATO umeanza leo mjini Bucharest nchini Romania. Rais George W Bush wa Marekani anahudhuria mkutano huo unaolezwa kuwa mkubwa kuwahi kufanywa na jumuiya hiyo. Mwandishi wetu Mkutano wa NATO utakuwa mgumu huku vita nchini Afghanistan vikitarajiwa kupewa kipaumbele.
Mkutano wa siku tatu wa jumuiya ya NATO mjini Bucharest nchini Romania unahudhuriwa na zaidi ya viongozi 50 wa dunia. Mkutano huo unatarajiwa kupitisha maamuzi makubwa kuhusu njia za kuvishinda vita nchini Afghanistan, kwa umbali gani kuipanua mipaka ya jumuiya ya NATO na vipi kurekebisha mahusiano mabaya na Urusi.
Mkutano wa NATO unaofanyika katika ikulu iliyojengwa na dikteta Nicolae Ceausescu, utakuwa wa mwisho kwa rais Bush na mwenzake wa Urusi, Vladamir Putin, ambaye amepangiwa kujumuika kwenye mazungumzo siku ya mwisho ya mkutano huo hapo keshokutwa Ijumaa.
Rais Bush amewasili mjini Bucharest akiwa ameandamana na mke wake Laura pamoja na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice.
Hotuba
Katika hotuba aliyoitoa mjini Bucharest rais Bush amishinikiza jumuiya ya NATO imalize vita dhidi ya watu wenye siasa kali nchini Afghanistan na kuitaka Urusi ijunge na mpango wa ulinzi dhidi ya makombora ambao amesema unahitajika kwa haraka kuzuia uwezekeno wa kitisho kutoka Iran. Rais Bush ametaka washirika wa NATO wapeleke wanajeshi zaidi nchini Afghanistan kupambana na watu wenye itikadi kali.
"Ikiwa tutapunguza shinikizo, watu wenye siasa kali watajenga tena ngome kote nchini na kuzitumia kuwatisha raia wa Afghanistan na kuwatisha watu wetu. Na hiyo ndiyo sababu kwa nini tutaendelea kukabiliana nao na kuwashinikiza. Na hiyo ndiyo sababu kwa nini tutashinda."
Rais Bush amesema jumuiya ya NATO iliyoundwa kukabiliana na utawala wa Soviet imemaliza jukumu lake na sasa inatakiwa iwe muungano wa kuchukua hatua za haraka duniani kote.
"Muungano wetu sharti udumishe lengo lake na umalize vita nchini Afghanistan, amesema rais Bush. Amekumbusha kwamba wiki mbili zilizopita Osama bin Laden alitoa ukanda wa video akitoa kitisho cha kufanya mashambulio mapya barani Ulaya na kuonya kuhusu haja ya kuyazingatia kwa makini maneno hayo ya adui.
Rais Bush amewasili Romania akitokea Ukraine, nchi inayotaka kujiunga na jumuiya ya NATO na anapanga kwenda Croatia ambayo pia inataka kuwa mwanachama wa NATO baada ya mkutano kumalizika hapo siku ya Ijumaa. Hapo kesho, ikiwa siku ya pili ya mkutano wa Bucharest, jumuiya ya NATO itajadili na kuamua kuhusu unachama wa Croatia, Albania na Macedonia.
"Kesho jumuiya ya NATO itapitisha uamuzi wa kihistoria kuhusu uanachama wa mataifa matatu ya Balkan; Croatia, Albania na Macedonia. Marekani inaunga mkono kwa dhati kuzikaribisha nchi hizi zijiunge na NATO. Zimefanya mageuzi, zimejenga jamii huru na wananchi wake wanastahili usalama unaotolewa na NATO"
Croatia ina hakika kukaribishwa kujiunga na jumuiya ya NATO kwenye mkutano wa Bucharest lakini uanachama wa Albania na Macedonia bado haujakuwa na uhakika.
Viongozi 26 wa nchi wanachama wa jumuiya ya NATO wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa mjini Bucharest utakaolindwa na maafisa 10,000 wa polisi. Mkutano huo umegubikwa na hatua ya Urusi kupinga maombi ya Ukraine na Georgia kutaka kujiunga na jumuiya ya NATO na mipango ya Marekani kujenga mfumo wa ulinzi wa makombora nchini Poland na jamhuri ya Cheki.
Rais Bush amesema mfumo huo ni lazima ujengwe barani Ulaya na kusema atamhimiza rais Putin aacche kuupinga wakati watakapokutana huko Sochi mwishoni mwa juma hili.
"Katika mazungumzo yetu nitasisitiza kwamba mpango wetu wa ulinzi dhidi ya Marekani si kwa ajili ya ulinzi dhidi ya Urusi kama vile ambavyo jumuiya mpya ya NATO tunayoijenga hailengi kutoa ulinzi dhidi ya Urusi. Vita baridi viliisha! Urusi si adui yetu! Tunaandaa uhusiano mpya na Urusi kuhusu usalama ambao msingi wake haupo katika maangamizo ya pamoja."
Hii leo rais Bush atasafiri kwenda katika mji wa mapumziko wa Neptune katika bahari nyeusi kufanya mazungumzo na rais wa Romania, Traian Basescu. Serikali ya Romania inaitazama ziara ya Bush kama ishara kwamba Marekani inalipa umuhimu mkubwa eneo la bahari nyeusi ambako imekuwa na wanajeshi wake tangu mwaka jana wakati wa msimu wa kiangazi.