Mkutano wa kilele Afrika, Marekani waanza
4 Agosti 2014Tayari viongozi wakuu kadhaa wa Afrika wameshawasili mjini Washington, akiwemo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye alikuwa na mazungumzo na raia wa nchi yake wanaoishi hapa Marekani. Vile vile marais wa nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na Kati tayari wamepiga kambi kwenye hoteli za Washington, kabla ya mkutano wa kilele unaotarajiwa Jumatano.
Wizara ya Nje ya Marekani inasema kwa ujumla ni marais 47 watakaohudhuria mkutano huo, huku Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na mwenziwe Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone wakifuta ziara yao kutokana na ugonjwa wa Ebola katika nchi zao. Wengi miongoni mwa marais hao wamekuja na wake zao.
Ajenda za mkutano
Ratiba ya mkutano huu wa siku tatu inaonesha kuwa leo Jumatatu (4 Agosti) marais wote watakutana na maseneta pamoja na wawakilishi wa bunge la Marekani kwenye jengo la bunge, Capitole. Baadaye kutafanyika mkutano wa mashirika ya kiraia kutoka Afrika na maafisa wa serikali ya Marekani na vilevile Waafrika wanaoishi Marekani.
Mikutano hiyo kwa pamoja itazungumzia utawala bora barani Afrika. Hata hivyo, mkutano unaosubiriwa kwa hamu sana hii leo ni ule unaohusu mradi wa umeme barani Afrika, "Power Africa", ambao ulianzishwa na Rais Obama mwaka jana.
Jumanne marais wote watakuwa na chakula cha jioni na Rais Obama na mkewe, Michelle, kwenye ikulu ya White House. Kilele cha mkutano huo ni hapo Jumatano (6 Agosti) kwa mkutano baina ya Rais Obama na marais wote wa nchi za kiafrika, ambao utakuwa na vikao vitatu kwa wakati mmoja - kikao cha kwanza kitahusu maswala ya uchumi na uwekezaji barani Afrika, cha pili kitahusu amani na usalama wa nchi za Kiafrika na mwishowe itakuwa ni kikao kitakachojadili maswala ya utawala bora barani Afrika.
Obama kutokukutana na kiongozi mmoja mmoja
Tayari maafisa wa Marekani wameelezea kwamba hakutokueko na mazungumzo ya kipekee baina ya Rais Obama na marais wa Afrika. Wadadisi wamesema kwamba mkutano huu unalenga hasa kuboresha uwekezaji wa Marekani barani Afrika na vilevile kuzuia kujikita kwa nchi zingine tajiri mfano wa China barani Afrika.
Lakini maafisa wa serikali ya marekani wamelezea kwamba mkutano huo unalenga siyo kupanga mikakati kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, bali ushirikiano wa dhati baina ya pande hizo mbili kwani Afrika ni bara ambalo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
Viongozi wa mashirika ya kiraia wanaitaka Marekani kuwashinikiza viongozi wa Kiafrika kuhusu utawala bora na matumizi ya rasilimali za bara hilo kwa manufaa ya watu wake.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Washington
Mhariri: Mohammed Khelef