Mkutano wa kilele kuhusu Afrika
14 Juni 2017Mada nyingine ni kuhusu jinsi alivyohojiwa mwanasheria mkuu wa Marekani Jeff Sessions na kamati ya baraza la Seneti hapo jana.
Mada kuhusu mkutano wa kilele kuhusu bara la Afrika uliomalizika jana mjini Berlin hapa Ujerumani. Mhariri wa gazeti la Die Rheipfalz anaandika kwamba , kwanini misaada ya maendeleo haileti maendeleo? Mhariri anaendelea kuandika
"Ni kwasababu , kwanza ; Ni wanasiasa pekee na wale wenye uwezo kiuchumi ndio wanafaidika zaidi katika nchi hizo zinazopokea misaada. Kwa wale mamilioni ya Waafrika ambao wakati wote wako katika hali ngumu ya maisha hawapati chochote. Kwa upande wa nchi wafadhili , kitengo cha misaada ya maendeleo , ni chombo cha kujinufaisha. Ndio sababu juhudi za Merkel zina kiini cha kushindwa, kwa kuwa hazihusiani kabisa na maendeleo. Ukweli ni kwamba wanataka kuwazuwia watu wanaotaka kuhama kutoka bara la Afrika kuja Ulaya. Unaweza mtu kusema hilo, na Merkel anapaswa kusema hivyo sio kujaribu kuleta matumaini ambayo hayapo."
Msingi wa hamasa mpya kuhusu bara la Afrika ni nyingine kabisa, anaandika mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung kuhusiana na mkutano huo wa kilele kwa ajili ya bara la Afrika. Mhariri anaendelea ....
"Ni kuhusu kuzuwia uhamiaji. Waafrika hawatakiwi kuja kwetu, wanatakiwa kutafuta kazi katika nchi zao na wabakie huko. Ndivyo wanavyofikiri watu wa huku kaskazini. Utaratibu sio kuwakataa kabisa , lakini umo katika makosa yetu. Ukuaji wa uchumi hautazuwia uhamiaji, badala yake unahimiza. Waafrika wengi wamehamia nchi za nje katika wakati wa ukuaji mkubwa wa uchumi hivi karibuni kuliko wakati mwingine wowote. Ghana , Senegal , Nigeria, si kitu cha bahati mbaya kwamba watu wengi walioomba hifadhi wanatoka nchi hizi zilizoneemeka. Masikini wengi hawana fedha ama nguvu za kuweza kufanya safari za kuhamia nchi za nje. Inahitaji zaidi ya ukuaji wa uchumi , kwa watu kubakia katika nchi zao. Wakati kundi la G20 linalenga kuwekeza katika sekta binafsi kama nguvu ya kuleta maendeleo katika bara la Afrika, haina maana ya kuondoa kiini cha matatizo , ambayo ni rushwa."
Kuhusu mada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani wa serikali za majimbo nchini Ujerumani kuzungumzia kuhusu usalama wa ndani kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Septemba , mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung anaandika:
"Sheria zilizopo za usalama haziwezi tena kuufanya ulimwengu kuwa salama. Tunapata uzoefu huo na mawaziri wa mambo ya ndani kutoka serikali kuu na za majimbo watakuwa waangalifu sana kuweza kulichokoza suala hilo, kwa kuwa wakiamua kuleta sheria mpya huenda wakawaweka wananchi katika hali ngumu. Ni somo pia kutokana na tukio lililofanywa na mhamiaji Amri , ambaye kama sio kushindwa kushindwa kwa maafisa wa usalama kumdhibiti mambo yaliyotokea yasingetokea."
Gazeti la mjini Mainz , Allgemeine Zeitung , linaandika kuhusu mada hiyo kwa kusema..
"Baadhi ya nyakati kunaonekana wazi kabisa hali ya udhaifu katika serikali ya shirikisho . Kutokana na mbinu zinazotofautiana kwa maafisa wa ulinzi wa amani katika jeshi la polisi wamewafanya wahalifu kuwa na nguvu zaidi. Hali hii imejengeka kwa miaka mingi , iwapo itabadilika, haijulikani. Kila jimbo linahitaji sheria zake za jeshi la polisi kuweza kujilinda, ambazo zinaweza pia kutumika nchi nzima, utaratibu wa adhabu unaweza kuainishwa na kuwa na nguvu zaidi."
Kuhusu kuhojiwa kwa mwanasheria mkuu wa Marekani katika kamati ya baraza la seneti jana , mhariri wa gazeti la Landeszeitung la mjini Lüneburg anaandika ......
"Kabla hata mwanasheria mkuu wa serikali ya Marekani Jeff Sessisions kusema kitu ilikuwa tayari ni wazi , kwamba atabadilisha mwelekeo wa athari zinazotokana na Trump. Mwelekeo ni kuhusu mchanganyiko wa madaraka yake kama rais na biashara zake za mahoteli. Kama kutakuwa na mashitaka , huenda Trump akalazimishwa kuweka wazi marejesho ya matumizi yake pamoja na kodi. Hii inapelekea kuwapo na fursa ya kumshitaki. Na hapa panahitajika theluthi mbili ya wabunge wa baraza la seneti. Lakini wabunge wa chama cha republikan ambao hawamtetei Trump ni wengi pia. Hii ni kutokana na sababu moja muhimu. haijawahi kutokea wananchi wengi wa Marekani katika muda mfupi tangu rais kuingia madarakani kuwa hawana imani na kazi yake."
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Yusuf Saumu