1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano Umoja wa Ulaya, Amerika Kusini kwenye mkwamo

18 Julai 2023

Mkutano wa kilele baina ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Amerika ya Kusini uliokuwa umetegemewa kuimarisha mahusiano baina ya pande hizo umegeuka kuwa mzozo wa kidiplomasia juu ya vita nchini Ukraine.

EU-CELAC Gipfel in Brüssel
Picha: YVES HERMAN/REUTERS

Wanadiplomasia wa pande hizo mbili walikesha hadi usiku wa manane kuamkia leo kusaka angalau tamko la pamoja la kuilaani Urusi kwa uvamizi wake dhidi ya Ukraine, lakini mazungumzo yalikwama kutokana na upinzani wa mataifa ya Amerika Kusini kama vile Cuba, Venezuela na Nicaragua. 

"Litakuwa jambo la aibu kwamba hatuwezi hata kusema kwamba kuna uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Ni ukweli. Na sipo hapa kuja kuiandika upya historia." Alisema Waziri Mkuu wa Luxembourg, Xavier Bettel, alisema kwa hasira.

Soma zaidi: Ulaya kuwekeza Amerika ya Kusini na Karibiki

Mwenzake wa Ireland, Leo Varadkar, alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba "baadhi ya wakati ni bora kutokuwa na hitimisho lolote kuliko kuwa na lugha ambayo haimaanishi chochote."

Varadkar aliongeza kuwa haikubaliki mkutano huo wa kilele kutokuwa na tamko la wazi na madhubuti la kuikemea Urusi kwa kile ambacho mataifa ya Umoja wa Ulaya yanakihisabu kuwa ni uchokozi dhidi ya Ukraine.

Mkutano uliosubiriwa kwa hamu

Mkutano huu ambao ulisubiriwa kwa miaka minane mizima tangu ulipomalizika ulioutangulia, uligeuka kuwa mkwamo juu ya nani wa kuanza mwanzo kuyazungumzia masuala ambayo mengi miongoni mwa mataifa 60 yanayohudhuria tayari yalishakubaliana kupitia kura zao kwenye Umoja wa Mataifa na taasisi nyengine za kimataifa.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep BorrellPicha: Florian Gärtner/imago images/photothek

Wakati mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yalitaka mkutano huo wa kilele kujikita kwenye miradi mipya ya kiuchumi na ushirikiano wa karibu zaidi ili kukabiliana na kitisho cha kutanuka kwa ushawishi wa China kwenye eneo lao, viongozi kadhaa wa Jumuiya ya Nchi za Amerika Kusini na Karibiani (CELAC) walikuja mezani na madai ya karne nzima juu ya uovu wa ukoloni na utumwa.

Soma zaidi: Borrell asema hatajarjii mafanikio makubwa kuhusu biashara huria

"Sehemu kubwa ya Ulaya ilikuwa na hadi leo bado ndiyo mfaidika mkubwa wa mahusiano haya ambapo Amerika Kusini na Karibiani yetu imekuwa na bado inakamuliwa," Waziri Mkuu wa visiwa vya St. Vincent na Grenadine, Ralph Gonsalves, ambaye ndiye rais wa Jumuiya ya CELAC.

Kuitetea Ukraine kidiplomasia na kuilaani Urusi imekuwa ada ya mataifa ya Umoja wa Ulaya, lakini kwa muda wote serikali nyingi za Amerika ya Kati na Kusini zimeamua kufuata msimamo wa katikati kwenye mzozo huo barani Ulaya, ambao kwao ni mmoja tu kati ya mingi inayoukabili ulimwengu.

Wachambuzi wanasema uwezekano wa mkutano huo kumalizika jioni ya leo bila ya makubaliano yoyote ya msingi ni mkubwa.

Vyanzo: AP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW