Mkutano wa kilele wa bara la Asia na Afrika umeanza leo mjini Jakarta.
22 Aprili 2005Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh anaiwakilisha nchi yake katika mkutano huo wa siku mbili, unaohudhuriwa na viongozi wasiopungua 50 kutoka mataifa mabalimbali. Mkutano huo unaadhimisha miaka 50 tangu kufanyika mkutano wa Bandung mwaka wa 1955.
Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, ametoa hotuba ya kuufungua mkutano huo, akizitolea wito nchi za mabara ya Asia na Afrika kuboresha uhusiano wa kiuchumi kati yao. Amewataka viongozi wanaohudhuria mkutano huo kujadili vipi Asia na Afrika zinaweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja badala ya kustarehe katika mkutano huo.
Yudhoyono amesema Asia na Afrika zimesahaulika katika mahusiano ya kimataifa, na ijapo imechukua miaka 50 kabla mkutano huo kufanyika, leo wana wa Asia na Afrika wanakutana pamoja kama watu wa tabaka moja maishani. Amesisitiza viongozi lazima wasahau yaliyopita na wagange yajayo. Wote kwa pamoja wanatakiwa kujadili maswala ya kuleta maendeleo katika mabara yote mawili katika siku za usoni.
Mkutano huo hatimaye unatarajiwa kutoa taarifa itakayotaka kuwepo ushirikiano, ahadi za kuboresha biashara na uwekezaji na kusisitiza umuhimu wa kuitanzua mizozo kwa njia ya mazungumzo. Lakini mizozo ya kidiplomasia barani Asia na maadui wake wa zamani ni maswala yanayougubika mkutano huo, ukiwemo mzozo kati ya China na Japan.
Waziri mkuu wa Japan, Junichiro Koizumi, ameomba msamaha kwa mateso yaliyofanywa na taifa lake katika mataifa ya Asia wakati wa vita vya pili vya dunia na kuahidi kuongeza mara mbili misaada barani Afrika katika muda wa miaka mitatu ijayo.
Amesema Japan itandaa mkutano wa kimataifa kuhusu maendeleo barani Afrika mwaka wa 2008. Serikali ya Tokyo imetoa dola bilioni 24 za misaada kwa mataifa ya Afrika tangu mwaka wa 1960. Wadadisi wanasema hii ni njia ya kuziongezea nguvu juhudi zake za kutaka kiti cha kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Koizumi atakutana hapo kesho na rais wa China, Hu Jintao, kandoni mwa mkutano huo wa Jakarta, kujaribu kuutanzua mzozo kati ya mataifa hayo mawili. Rais Jintao katika hotuba yake hakuitaja Japan, lakini akaahidi China itaendela kuwa mwanachama wa mataifa yanayoendelea na itakuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine. Ametoa wito ya kuwepo ushirikiano kati ya mataifa hayo.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan, amewahimiza viongozi wa Asia na Afrika kuwa hodari na kuyaunga mkono mapendekezo yake ya kihistoria ya kuufanyia mabadiliko umoja wa mataifa. Akiwahutubia viongozi kutoka mataifa 100 yanayojumulisha thuluthi tatu za matifa yote ulimwenguni, Annan amesema anataka kuufanya mwaka huu wa 2005 kuwa mwaka wa mabadiliko kwa watu maskini na umoja wa mataifa.
Annan amewaalika marais, mawaziri wakuu na wafalme wanaokutana mjini Jakarta wahudhurie mkutano katika makao makuu ya umoja wa mataifa mjini New York, Marekani, kuhusu uchumi, usalama na haki za binadamu, utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu. Amesisitiza kwamba kila mmoja anatakiwa kuzingatia masilahi ya nchi yake na kwamba tunaishi katika ulimwengu mmoja tukiwa na hatima moja.
Amesema kuna umuhimu wa raslimali kugawanywa kwa mataifa yanayoendelea ili yaweze kujimudu katika maendeleo. Kila nchi tajiri inatakiwa kutoa asilimia 0.7 ya utajiri wake wa kitaifa kama msaada wa maendeleo kufikia mwaka wa 2015.
Annan amewaambia viongozi katika mkutano huo kuheshimu kumbukumbu za mkutano wa Bandung uliofanyika miaka 50 iliyopita, kwa kuyaendeleza malengo ya tukio alilolitaja kuwa la muhimu katika historia. Siku ya Jumapili wajumbe katika mkutano huo watasafiri hadi Bandung.