1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa G7 unafanyika Ufaransa

24 Agosti 2019

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema masuala ya kujadiliwa katika mkutano wa kilele wa mwaka huu wa kundi la nchi saba tajiri duniani, G7 ni mengi, yakiwemo biashara na mazingira.

Frankreich G7-Gipfel in Biarritz | Donald Tusk
Picha: Reuters/C. Hartmann

Akizungumza na waandishi habari mjini Biarritz, kusini mwa Ufaransa ambako mkutano huo wa kilele unafanyika, Tusk amesema mkutano wa mwaka huu utakuwa mtihani mgumu kwa umoja na mshikamano wa dunia huru na viongozi wake, ambapo masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na mvutano wa kibiashara na Marekani, Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya pamoja na kuungua kwa msitu wa Amazon.

'Vita vya kibiashara vitasababisha kushuka kwa uchumi, huku mikataba ya kibiashara ikichangia kukua kwa uchumi'', alisisitiza Tusk. Wasiwasi kuhusu vita vya kibiashara na mabadiliko ya tabia nchi unaongezeka wakati ambapo viongozi hao wa G7 wanakutana huku wakiwa na matumaini madogo kuhusu viongozi hao kufikia makubaliano ifikapo mwishoni mwa mkutano huo wa siku tatu.

Baada ya kuwasili nchini Ufaransa kuhudhuria mkutano huo wa kilele wa G7, Rais wa Marekani, Donald Trump na viongozi wa Umoja wa Ulaya walitupiana maneno ya vitisho kuhusu vita vya kibiashara.

Mivutano ina madhara

Rais wa Ufaransa, Emannuel Macron, ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amesema lengo lake kuu ni kuwashawishi washirika wao wote kwamba mivutano hasa ule wa kibiashara ni jambo baya kwa kila mmoja.

Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Reuters/L. Marin

Aidha, mchana wa leo Trump na Macron walikutana kwa chakula cha mchana ratiba ambayo ilikuwa haijapangwa hapo awali, kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano wa kilele wa G7. Viongozi hao wawili walionekana katika kibaraza cha hoteli du Palais, Biarritz, ikiwa ni siku moja baada ya Trump kurudia kutoa kitisho kuhusu ushuru katika vimnyo ya Ufaransa katika kulipiza kisasi cha kodi mpya katika kampuni kubwa za teknolojia za Marekani.

Chakula hicho cha mchana kati ya viongozi hao wa Ufaransa na Marekani kinaonekana kuwa jaribio la Macron kuweka mwanzo mzuri wa mkutano huo wa G7 baada ya kuwepo vita vya maneno ambapo Trump na viongozi wa Umoja wa Ulaya walirushiana vitisho vya vita vya kibiashara.

Akizungumza na waandishi habari, Macron alimuita Trump kuwa ni ''mgeni maalum sana''. Rais huyo wa Ufaransa amesema watajadiliana masuala ya kimataifa ikiwemo mkwamo wa Iran kuhusu dhamira yake ya silaha za nyuklia na kusisitiza kwamba ushirikiano madhubuti unahitajika.

Kwa upande wake Trump amesema kuwa yeye na Macron wamekuwa marafiki wa muda mrefu na hadi sasa mambo yanakwenda vizuri. ''Wakati mwingine mambo yanakuwa hivi, lakini tuna uhusiano mzuri sana'', alifafanua Trump. Rais huyo wa Marekani amebainisha kuwa ana matumaini watafikia masuala mbalimbali mwishoni mwa juma hili.

Macron ataka hatua zichukulie msitu wa Amazon

Ama kwa upande mwingine Rais Macron ameongoza sauti za viongozi wa kimataifa katika kumuwekea shinikizo Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro kuhusiana na moto unaoendelea kuutekeza msitu wa Amazon, akimwambia kuwa Ufaransa itazuia juhudi za kufikia makubaliano muhimu ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini, kama hatochukua hatua.

''Viongozi wa kundi la G7 sio tutatawasilisha tu ombi, bali tutazihamasisha nchi zote zenye nguvu, lakini katika ushirikiano na nchi za Amazonia kuhakikisha tunaudhibiti huu moto na kuwekeza katika ukataji miti'', alibainisha Macron.

Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema anaunga mkono mazungumzo kuhusu moto kwenye msitu wa Amazoni wakati wa mkutano wa kilele wa G7, lakini hakubaliani na kuuzuia mkataba wa kibiashara wa Mercosur kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Amerika Kusini kwamba kutapunguza uharibifu katika msitu huo.

''Tutafanya kazi kuangalia namna ya kusaidia na kuunga mkono kwa kupeleka ujumbe wa wazi kwamba juhudi za dhati zinapaswa kuchukuliwa ili kuuzima moto katika msitu huo wa Brazil ambao ni chanzo kikubwa cha mvua na ambao umepewa jina "mapafu ya dunia" kutokana na umuhimu wake huo'', alisema Kansela Merkel katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video.

Wakati huo huo, maelfu ya watu wameandamana karibu na mji wa Hendaye kupinga kuhusu sera za kiuchumi na kimazingira, huku wakiwataka viongozi wa dunia kuchukua hatua katika suala zima la mabadiliko ya tabia nchi pamoja na masuala mengine.

Waandamanaji wanaoupinga mkutano wa kilele wa G7Picha: DW/B. Riegert

Waandamanaji wapatao 15,000 wanaoupinga mkutano wa G7 walikusanyika katika eneo hilo lililoko kwenye mpaka wa Ufaransa na Uhispania wakati viongozi wa madola yenye nguvu wakiwasili mjini Biarritz.

Waandamanaji hao wakiwemo wanaopinga ubepari, wanamazingira na makundi mengine wamekuwa wakimiminika katika mji huo wa kusini magharibi mwa Ufaransa kuonyesha upinzani wao kwa mkutano huo wa kilele. Idadi kubwa ya polisi imeweka doria kuzuia vurugu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW