Wakuu wa EAC kukutana leo Arusha, biashara kwenye agenda
21 Julai 2022Rais Samia Suluhu Hasan wa Tanzania, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Evariste Ndayishimiye wa Burundi, Salva Kiir wa Sudan Kusini na kwa mara ya kwanza rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi.
Pamoja na mambo mengine, watakuwa na jukumu la kuteua majaji wa mahakama ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa mwaka 2001.
Mkutano huu wa kawaida wa kisheria, pia utajadili utekelezaji wa soko huria la bidhaa na huduma miongoni mwa nchi wanachama pamoja na mwongozo wa jumla wa uhuru wa kusafiri, ambapo mchakato wake ulianza tangu miaka 10 iliyopita.
Wakuu hao wa nchi watawateua majaji wa mahakama ya Afrika Mashariki ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa kisheria ulioainishwa katika mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Marais hao pia wanatarajiwa kuzindua barabara ya mzunguko iliyopo Arusha Tanzania inayoziunganisha nchi za Tanzania na Kenya yenye urefu wa kilometa 42.4, ambayo pia inatajwa kuwa nyenzo muhimu ya kukuza biashara miongoni mwa mataifa hayo mawili.
Kwa mara ya kwanza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inashiriki mkutano huu kama mwanachama rasmi, huku matarajio ya ushirikiano hasa wa kibiashara yakiwa ni makubwa kutoka kwa nchi wanachama, kutokana na Kongo kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu ikilinganishwa na nchi nyingine za jumuiya hiyo.
-Veronica Natalis, DW Arusha.