Mkutano wa kilele wa Marekani na ASEAN
24 Septemba 2010Rais Barack Obama wa Marekani, ana azma ya kuimarisha zaidi usuhuba na nchi za Kusini-mashariki mwa Asia wakati wa mkutano wake na nchi hizo hii leo.Kikao chao kinafanyika wakati pakizuka changamoto za maswali ya usalama baharini kwa kuzidi kupata nguvu China.
Rais Obama anaandaa leo na mkutano wake wa pili wa kilele wa kundi la nchi za Jumuiya ya ASEAN na Marekani pembezoni mwa Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York. Na hii inafanyika siku moja tu baada ya kutangaza kwamba atafanya ziara yake ya Indonesia ilioahirishwa mara 2 hapo Novemba.
Rais Obama amefanya ushirikiano na Kusini-mashariki mwa Asia kuwa nguzo ya siasa zake za nje, na wakati wa ziara yake mwaka jana huko Asia alijiita "Rais wa kwanza wa Marekani kutoka eneo la bahari ya Pacifik".
"Tangu mwanzo wa utawala wake, tumejaribu kujenga uhusiano na nchi za ASEAN"-alisema Jeff Bader, mkurugenzi wa Rais Obama kwa bara la Asia kuhusu maswali ya usalama wa taifa.
Kikao cha leo cha masaa 2 kinatazamiwa kutuwama juu ya maswali ya biashara na uwekezaji , usalama wa eneo la Mashariki ya Asia na mifumo ya uchumi pamoja na juhudi za muda mrefu na zisizofanikiwa bado kuishinikiza Myanmar ili igeuze mkondo wa siasa zake.
Kikao cha leo, kinafanyika wakati mvutano unazidi baina ya majirani 2 wakubwa barani Asia, China na Japan, kuhusu kunyan'ganyia ardhi katika pwani ya Kusini mwa China. China inashikilia kumiliki visiwa tajiri kwa mali-asili vya Spratly na Paracel viliopo huko.Lakini, wanachama wa kundi la ASEAN, kama vile Philipines, Vietnam, Malaysia, Brunei pamoja na nchi isio-mwanachama, Taiwan, nazo pia zinatoa madai yao juu ya visiwa hivyo.
Bader aliarifu kwamba, Rais Obama kwa ufupi, alizungumzia swali hilo na waziri-mkuu wa china Wen Jiabao, walipokutana mjini New York pembezoni mwa kikao cha Baraza Kuu la UM hapo jana.Baadhi ya wachunguzi ,wanatarajia mkutano huu wa leo utatoa taarifa itakayosisitiza juu ya kuwapo kwa uhuru wa nyendo za safari za meli katika pwani ya Kusini mwa China.
Ikiutazamia mkutano huu wa New York, China imeionya Marekani, juzi isijiingize katika mzozo huu.Kikao cha leo, kinafuata kile cha kila mwaka cha mwaka uliopita nchini Singapore pamoja na nchi 10 za Kusini-mashariki mwa Asia.
Mwezi ujao katika mkutano mwengine na eneo hilo la Kusini-mashariki mwa Asia, waziri wa nje wa Marekan, bibi Hillary Clinton, atahudhuria mkutano wa kilele juu ya usalama huko Hanoi, Vietnam.Rais Barack Obama, anatarajiwa kuhudhuria kikao kama hiki kuanzia mwakani 2011.
Mwandishi: Ramadhan, Ali/ AFPE
Mhariri: Miraji Othman