Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wahamishiwa Addis Ababa
21 Juni 2012Umoja wa Afrika umeuhamishia mkutano wake wa kilele mwezi Julai katika mji mkuu wa Ethiopia baada ya Malawi kuzuwia kushiriki kwa Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir, anayetakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC.
Mwezi uliopita, Malawi iliuomba Umoja wa Afrika kumzuwia rais Bashir asishiriki, ikisema hilo litaathiri uchumi wake unaotegemea msaada kutoka nje.
Mwaka jana Malawi iliwakasirisha wafadhili wake wa kimataifa ambao wamekuwa wakifidia 40 asili mia ya bajeti ya nchi hiyo ilipomkaribisha Rais Bashir, wakati wa utawala wa Rais wa zamani, Bingu Wa Mutharika, aliyefariki dunia mwezi Aprili.
Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema sasa mkutano huo wa kilele wa 19 utafanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Ababa. Rais Bashir anatuhumiwa kupanga mauaji na maovu mengine dhidi ya binaadamu katika jimbo la Darfur.
Mwaka 2009, viongozi wa nchi za Afrika walilikataa ombi la mahakama ya kimataifa kumkamata kiongozi huyo wa Sudan, wakisema hatua hiyo itahujumu juhudi za kusuluhisha migogoro kadhaa ya ndani ya Sudan. Pia waliilaumu mahakama hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuwaandama waafrika pekee.