Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika
25 Julai 2010Mada kuu itakayojadiliwa na viongozi wa Umoja wa Afrika katika mkutano wao inahusika na Somalia, hasa kufuatia mashambulio yaliyoua watu 76 mjini Kampala. Inasemekana kuwa mashambulio hayo yalifanywa na wanamgambo wa Kisomali Al- Shebab. Viongozi hao walibakia kimya kwa dakika mbili kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo la Julai 11.
Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi nchi inayoshika wadhifa wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amewalaani vikali wahusika wa shambulio hilo.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir hakuhudhuria mkutano huo wa kilele. Mapema mwezi huu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliongezea mashtaka ya mauaji ya kimbari dhidi ya Rais Bashir, kwa hivyo Uganda iliyo mwanachama wa mahakama hiyo, ingepaswa kumkamata kiongozi huyo wa Sudan.
Mwandishi:P.Martin/AFPE
Mhariri: M.Dahman