Mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya na Afrika Magazetini
1 Desemba 2017Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Abidjan nchini Côte d'Ivoire ndio uliohodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii. Hata hivyo lakini hali nchini Zimbabwe baada ya kung'olewa madarakani Robert Mugabe nayo pia imezingatiwa.
Tunaanzia na mkutano wa tano wa viongozi wa Umoja wa ulaya na wenzao wa Afrika mjini Abidjan, mji mkuu wa kiuchumi wa Côte d'Ivoire. Mada kuu ilihusiana na jinsi ya kulivunja nguvu wimbi la wahamaji na hasa baada ya kufichuliwa ripoti kuhusu jinsi wahamaji hao wanavyyopigwa mnada katika masoko ya utumwa nchini Libya. Magazeti takriban yote na majarida ya humu nchini yameripoti kuhusu kisa hicho na kumulika mazungumzo ya Abidjan. Frankfurter Allgemeine linahisi mkutano huo ulikuwa fursa nzuri kwa Côte d'Ivoire. Frankfurter Allgemeine linachambua jinsi mada mbili kuu zilizohodhi mkutano huo, Vijana na Uhamaji zinavyoingiliana. Na ndio maana linaandika gazeti hilo la mjini Frankfurt dhamiri za viongozi 28 wa Umoja wa ulaya na wenzao 55 wa Afrika zilikuwa kusaka njia ya pamoja kuzuwia wimbi la wahamaji.
Frankfurter Allgemeine linakumbusha zaidi ya asili mia 60 ya wakaazi wa Afrika wana umri wa chini ya miaka 25, idadi ya wasiokuwa na kazi miongoni mwa vijana hao, kwa mujibu wa Umoja wa Afrika inafikia thuluthi moja. Kwamba wimbi la wahamaji litaendelea, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine, si suala la kuuliza kwasababu vijana hawaoni ishara ya matumaini mema katika nchi zao. Na ndio maana mpango wa mkakati uliopitishwa katika mkutano wa Malta, November mwaka 2015 umefufuliwa. Mjini Abidjan, Umoja wa ulaya umeahidi vitega uchumi vya kibinafsi vya Euro bilioni 44 ili kusaidia kuinua maendeleo ya kiuchumi, miundo mbinu, hifadhi ya mazingira na elimu. Kwa namna hiyo linamaliza Frankfurter Allgemeine, Umoja wa Ulaya unategemea kuwapatia matumaini mema vijana wa Afrika na kupunguza wimbi la wahamaji wanaoelekea Ulaya.
Utajiri usiokuwa na kifani wa Mugabe
Zimbabwe imejipatia rais mpya baada ya mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, Robert Gabriel Mugabe kukubali kung'atuka kufuatia shinikizo la wanajeshi. Ameiacha nchi hiyo katika hali fukara lakini mwenyewe "ni tajiri kupita kiasi" linaandika jarida la der Stern. Jarida hilo linanukuu kauli mbiu ya aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi ya jamhuri ya umma wa China Mao Zedong aliyesema mwaka 1949 "ufanisi wa nchi unategemea jinsi viongozi wanavyotosheka na kile haba wanachokipata". Der Stern linasema Mugabe ameisahau kauli hiyo.
Ingawa fedha za China na bunduki za Kalashnikov ndizo ziliopelekea Mugabe kuingia madarakani mwaka 1980, lakini mtindo wake wa maisha umebadilika kila miaka ilipozidi kupita, badala ya kuendeleza mtindo wa kimapinduzi ameamua kufuata wa kibepari. Jarida la der Stern linaorodhesha miliki za Mugabe ambazo ni pamoja na ndege za binafsi, magari ya anasa, makasri ya fakhari, mashamba aliyojimilikisha bila ya kutaja milki ya mkewe Grace . Utajiri huo uliokithiri hautatetereka licha ya kung'olewa madarakani, linamaliza kuandika jarida la der Stern linalokumbusha jinsi wananchi walio wengi wa Zimbabwe wanavyotaabia maiasha.
Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatufikisha Angola ambako mhariri wa gazeti la Süddeutsche anammulika binti ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Isabel dos Sanatos anaetajikama kuwa mwanamke tajiri kupita wote barani Afrika. Ingawa Isabel dos Santos amelazimika hivi sasa kujiacha kiti chake kama mkuu wa shirika la mafuta la nchi hiyo, hata hivyo ushawishi wake nchini humo haujapungua.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dwelle.de/BASIS/PRESSER/ALL PRESSE
Mhariri:Josephat Charo