1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya

24 Oktoba 2013

Viongozi wa serikali na nchi 28 za Umoja wa Ulaya wanakutana kwa siku mbili mjini Brussels ikiwa ni wiki kadhaa baada ya janga la kuangamia wakimbizi katika kisiwa cha Lampedusa.

Kansela Merkel , rais wa baraza la EU Herman Van Rompuy na Mkuu wa sera za nje za EU Catherine Ashton
Kansela Merkel , rais wa baraza la EU Herman Van Rompuy na Mkuu wa sera za nje za EU Catherine AshtonPicha: Reuters

Katika mwaliko wa mkutano wa kilele uliotolewa na rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, suala la wakimbizi katika ulaya ya Kusini limetajwa kwa mukhtasari tu. Aidha katika maazimio ya mkutano huo wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels ambayo tayari yameshatolewa kama rasimu, kisa cha Lampedusa katika bahari ya Mediterenia hakijachukuwa dhima kubwa. Viongozi wa serikali na nchi 28 za Umoja wa Ulaya wanakutana kwa siku mbili mjini Brussels. Mkutano huu unafanyika baada ya janga la kuangamia wakimbizi katika kisiwa cha Lampedusa kuzusha sauti za ukosoaji kuelekea sera ya Umoja wa Ulaya katika suala hilo la wakimbizi.

Suala la wakimbizi

Kwa waziri mkuu wa Italia, Enrico Letta hatua za Umoja wa Ulaya kuelekea suala hilo la wakimbizi hazitoshi. Baada ya mamia ya wakimbizi kuzama kufuatia ajali ya boti waliyokuwa wakisafiria katika kisiwa cha Lampedusa mwezi huu, waziri mkuu huyo wa Italia anatazamiwa kuwatia shime viongozi wenzake kutafakari suala la kugawana wakimbizi barani Ulaya.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mojawapo ya mikutano yao ya kilelePicha: Reuters

"Kuna baadhi ya nchi ambazo zinatuunga mkono. Baadhi ya nyingine zinafanya mambo kinyume na tunavyofanya sisi. Ni kwa nini tunataka suala hili lishughulikiwe katika ngazi ya Ulaya ni kwa sababu ndiko tunakofikia msimamo wa pamoja. Kwa mfano katika mwaka wa 2014 wakati Ugiriki na Italia zitakapochukuwa uwenyekiti wa Umoja wa Ulaya pamoja na kamisheni ya Umoja huo na baraza zitabidi kufanya kazi kwa pamoja kushughulikia suala hili''

Kauli ya Letta imetolewa wiki moja baada ya mkasa wa Lampedusa pale walipotembelea pamoja na rais wa Halmashauri ya Umoja huo, Jose Barroso, kisiwa hicho cha Italia kilichoko nje ya pwania ya Afrika Kaskazini.

Ujerumani pamoja na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya Kaskazini zinatarajiwa kudokeza katika mkutano huo juu ya suala la taratibu za uhamiaji katika Ulaya ambazo zilidurusiwa katika kipindi cha msimu wa joto. Nchi hizo zinategemewa kuzungumzia kile kinachojulikana kama sheria za Dublin ambazo kimsingi zinawalazimisha wanaoomba ukimbizi kuomba kinga katika nchi ya kwanza waliyofikia.

Misimamo

Duru kutoka serikali ya Ujerumani zimedokeza kabla ya mkutano huu wa kilele kwamba tayari limeshaundwa jopo la maafisa wa Umoja wa Ulaya pamoja na mawaziri ambao watakutana hii leo kwa mara ya kwanza likiwa na jukumu la kutowa ushauri juu ya njia zinazostahili kufuatwa katika suala la uokozi wa baharini na kuhusu ushirikiano wa karibu na nchi ambako wanatokea wakimbizi wanaoingia Ulaya.

Kisiwa cha Lampedusa - August 20, 2009 kiasi wakimbizi haramu 75 kutoka Afrika walifarikiPicha: picture-alliance/ROPI

''Nataraji kwamba Halmashauri ya Umoja wa Ulaya itafunguwa njia ya kupatikana msimamo wa pamoja wa uwajibikaji pamoja na sera ya kudhibiti uhamiaji katika kiwango cha Ulaya. Hakuwezi kuweko miujiza au mafanikio ya haraka haraka kwa sababu tatizo ni kubwa na linahitaji hatuwa madhubuti kuokowa maisha ya watu''

Kwa upande wa Ujerumani Martin Schulz ambaye ni rais wa Bunge la Ulaya kutoka chama cha SPD amedai mara kadhaa katika mahijiano kwamba Ujerumani inabidi kubeba jukumu kubwa la kuwapokea wakimbizi zaidi pamoja na wahamiaji ambao wanazidi kuingia Ulaya kwa kupitia bahari ya mediterenia.Hata hivyo waziri wa mambo ya nje anayemaliza muda wake Guido Westerwelle kutoka FDP amekiri katika mkutano uliopita wa mawaziri huko Luxembourg siku ya Jumatatu Ulaya haipaswi kupuuza tatizo hili.

''Ulaya haipaswi kuangalia kando na kupuuza .Hii ni hali ngumu na sio tu kwa nchi husika lakini ni tatizo hata kwa watu wanaohusika katika tatizo hili.Nataraji kwamba agenda hii itajadiliwa katika mkutano huu wa Kilele.Hili ni suala lisiloweza kuepukika.''

Uchumi

Aidha masuala ya kiuchumi pia yanatazamiwa kuzungumziwa kwa kina katika mkutano huo huku suala la mikataba ya mafungamano ya pamoja ya tume ya Umoja wa Ulaya likitarajiwa kuchukuwa nafasi ambapo Ujerumani inapania kupigia debe mageuzi kadhaa wakati baadhi ya nchi zikiwa na msimamo wa kuikosowa hatua hiyo.

Mwandishi/Riegert, Bernd (DW Brüssel)/Saumu

Mhariri:Josephat Charo

LINK: http://www.dw.de/dw/article/0,,17179150,00.html

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi