1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa juu ya maji wazinduliwa mjini Stokholm Sweden

Gregoire Nijimbere21 Agosti 2006

Unafunguliwa leo mjini Stokholm Sweeden mkutano wa kimataifa wa wiki nzima kuhusu swala zima la matumizi ya maji duniani. Wataalamu wameonya kuwa kuna athari maji yakakosekana kabisa mnamo miaka 50 ijayo ikiwa hatua mpya hazotochukuliwa kuboresha uhasibu wake.

Tatizo la maji nchini Uchina
Tatizo la maji nchini UchinaPicha: AP

Kulingana na makisio ya wataalamu, kutakuwa na ongezeko la watu kati ya bilioni 2 na bilioni 3 hadi mwaka wa 2050. Kwa hiyo kutokana na hali kwamba maji tayari ni haba kwa baadhi ya wakaazi duniani, ni budi ipangwe mikakati mipya ya kufanya uhasibu wa asili hiyo mahitajio muhimu uwe bora kuliko ilivyo hivi sasa. Mikakati hiyo ni muhimu ili dunia ya kesho isikose kabisa maji. Matatizo ya maji yanaripotiwa katika nchi tarkiban zote ila kwa njia tofauti kama anavyoelezea Andres Berntell, mkurugenzi wa taasisi ya maji ya mjini Stokholm.

„ Hata katika nchi za magharibi kuna sehemu zinazokabiliwa na matatizo kuhusu ugavi wa maji. Pamoja na hayo kiwango cha ubora ya maji hayo ni cha chini. Tatizo hili lipo katika sehemu za mediterania barani Ulaya na kusini mwa Marekani.

Miji tajiri kama Sydney na Huston inatumia maji zaidi kuliko mazingira ya asili yanavyoweza kufidia. Jambo linalopasa kufanyika ni kutumia maji kwa uangalifu na kwa ufanisi. Katika sehemu hizo watu wanatambua ulazima wa kufuata sera hiyo wakati sisi katika nchi za kaskazini, tunajiemndekeza kutokana na maji kupatikana kwa wingi. Yaelekea hatutambui vizuri, ni kwa kiasi gani maji safi ni muhimu kwa uhai wa mwanadamu katika nchi zinazoendelea.“

Wataalamu ambao walifanya utafiti kuhusu hali ya matumizi ya maji na ambao timu yao itashiriki kwenye mkutano huo wa kimataifa wa mjini Stokholm Sweeden wameonya katika matokeo yao kwamba kuna hatari.

„Tayari theluthi ya wakaazi duniani wanaangaika kwa njia moja ama nyingine kupata maji. Hali ni ngumu zaidi kuliko inavyofikiriwa“, amesema Frank Rijsberman, mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kimataifa inayohusika na uhasibu wa maji IWMI.

Mfano wa kusikitisha ni kwamba nchi kama Uchina na Australia zimeanza kukosa maji katika sehemu fulani huku mafuriko yakiyavamia maeneo nchini India. Kiongozi huyo ambae ndiye alifanya uratibu wa shughuli za utafiti ulioendeshwa na wataalamu 700 alifanya makadirio ya matumizi ya maji kwa ajili ya kilimo na kugundua kwamba asili mia 74 ya maji yanayotumiwa na binaadamu ni kwa ajili ya kilimo.

Kaona kwamba maeneo yanayokosa maji ni kutokana na sababu mbili. Mmoja ni kwamba kuna maeneo yanayokosa maji kutokana na matumizi ya kupita kiasi, na hivyo kusababisha kushuka kwa akiba ya maji chini ya ardhi au mito kukauka. Katika maeneo mengine, maji ni haba kwa sababu wakaazi wa maeneo hayo hawana uwezo wa kiufundi na vifaa kuweza kukusanya maji ya nvua au kuelekeza maji ya mito kwa ajili ya matumizi ya nyumbani au mashambani.

Kwa vyovyote vile, uhaba wa maji unaoshuhudiwa hivi sasa katika sehemu kadhaa duniani, unatokana kwa sehemu kubwa na makasa katika uhasibu wake na wala siyo ukosefu kabisa. Binaadamu wanahusika kwa asili mia 98 kulingana na wataalamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW