1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa kuhusu mustakbali wa Somalia wafanyika mjini Mogadishu

5 Septemba 2011

Viongozi wa Somalia wanakutana leo kwa siku ya pili ya mkutano wa kitaifa wa siku tatu ulioanza hapo jana katika mji mkuu Mogadishu.

Ujenzi mpya wa Somalia iliyovurugwa kwa vita ni changamoto kubwaPicha: dapd

Mkutano huo unalenga kujadili mustakabali wa taifa hilo ambalo limekumbwa na vita, na kuumaliza uongozi wa miaka saba wa serikali ya mpito ambayo imeshindwa kutimiza malengo yake.

Muda wa kufanya kazi kwa Serikali hiyo ya mpito ulipaswa kumalizika mwezi uliopita, lakini rais wa Somalia, Sharif Sheikh Ahmed, na spika wa bunge, Sharif Hassan Sheikh Aden, walitia saini mkataba mjini Kampala mwezi Juni wa kuwaongezea muda wa kuhudumu kwa mwaka mmoja zaidi.

Mazungumuzo hayo katika mji huo mkuu wa Mogadishu yataangazia kuboresha usalama, maridhiano ya kitaifa, katiba mpya, uongozi na marekebisho ya bunge.

Katika ufunguzi wa mazungumzo hayo, rais Sharif alisema ni siku hiyo ni ya kihistoria na anatumai kuwa mazungumzo hayo yataleta mawazo ya manufaa yatayoleta kikomo kwa matatizo ya Somalia.

Rais wa eneo la Puntland lililojitenga kutoka Somalia, Ibrahim Mohammed Mohamoud, kiongozi wa eneo la Galmudug linalojitawala, na wanachama wa kundi la waasi linaloiunga mkono serikali ya Somalia la Ahlu Sunna Wal Jamma pia walihudhuria mazungumzo hayo yaliyoandaliwa na umoja wa mataifa.

Mwakilishi wa umoja wa mataifa nchini Somalia, Augustine Mahiga, alisema kuwa wana mwaka mmoja kutimiza majukumu yaliyopewa kipaumbele na kwamba mchakato huo utatoa fursa ya kupatikana amani nchini humo ambayo haijakuwa kwa miaka ishirini.

Hata hivyo, viongozi kutoka eneo lililojitenga la Somaliland na waasi wa kundi la Alshabab ambalo limeapa kuipindua serikali hawakuwakilishwa kwenye mkutano huo.

Waasi wa kundi la Al ShababPicha: AP

Serikali ya mpito ya Somalia ilibuniwa katika nchi jirani ya Kenya mwaka 2004 na kupewa miaka mitano ya kufanyakazi ili kuleta maridhiano nchini Somalia, kuandika katiba mpya na kufanya chaguzi.

Lakini mizozo ya kila mara ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vimetatiza juhudi hizo, hivyo muda wa kazi ya serikali hiyo kuongezwa mara mbili . Pia imekuwa na marais wawili na mawaziri wakuu watano kwa kipindi hicho.

Serikali hiyo imeshindwa kuidhibiti Somalia isipokuwa maeneo machache ya mjini Mogadishu kutokana na mashambulio ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la Alshabab linaloungwa mkono na mtandao wa Alqaeda, na kuwepo kwake madarakani ni kutokana na juhudi za kikosi cha usalama cha umoja wa Afrika.

Bwana Mahiga ameonya kuwa usaidizi wa siku za usoni kwa serikali hiyo ya mpito utategemea jinsi itakavyotekeleza mipango hiyo mipya, na kuongeza kuwa mchakato huo utakapelekea kumalizika kwa serikali ya mpito na kutoa nafasi kwa serikali kamili.

Kuendesha serikali hiyo ya Somali kunawagharimu wafadhili kati ya dola milioni 50 na mia moja kwa mwaka, ilhali kikosi cha usalama cha Umoja wa Afrika kinachoilinda serikali hiyo kilicho na wanajeshi 9,000 kikigharimu dola milioni 400 kwa mwaka.

Serikali hiyo ya sasa ni miongoni mwa juhudi za kuleta mamlaka na udhibiti nchini humo tangu ilipotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1991na kungo´lewa kutoka madarakani rais Mohammed Siad Barre.

Mwandishi: Caro Robi/AFP

Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW