1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa kuisaidia Somalia

Sylvia Mwehozi
11 Mei 2017

Rais wa Somalia ameyaomba mataifa yaliyo na nguvu kumsaidia katika kupambana na ugaidi, rushwa na umaskini katika mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia uliofanyika London unaolenga kurejesha utulivu katika nchi hiyo.

Großbritannien Somalia-Konferenz
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Hill

Mohamed Abdullahi Mohamed amewaambia wajumbe waliokusanyika katika mkutano huo wa London kwamba taifa hilo lililovurugika kwasababu ya mgogoro linao uwezo wa kustawi kwa kutumia kipaji chake cha asili cha biashara ikiwa tu litaondokana na vikwazo vya njaa, uharamia na Waislamu wenye misimamo mikali.

Mkutano huo wa siku moja unaohudhuriwa na viongozi wa dunia, unatazamiwa kutoka na makubaliano mapya baina ya serikali ya Somalia na mtandao wa kimataifa wa kuisaidia nchi hiyo ili kuongeza kasi ya mchakato wa kiusalama, maendeleo na uchumi ifikapo mwaka 2020.

Taifa hilo la Afrika mashariki lililokumbwa na shida mara kadhaa limekuwa katika hali tete, liko chini ya utawala wa rais mpya, waziri mkuu na bunge kwa mwaka huu na mkutano huo unalenga kuleta misingi ya utulivu katika mchakato wa uchaguzi.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi MohamedPicha: REUTERS/F. Omar

Rais Farmajo kama anavyojulikana na wengi amesema kwamba anafahamu matarajio makubwa waliyo nayo raia wa Somalia juu yake hasa kuimarisha usalama, upatikanaji wa huduma za msingi kama vile afya na elimu. Na akaongeza kwamba utawala wake unafanya kazi bila kuchoka kufikia malengo ya kila mmoja, na wana matumaini ya kuboresha maisha ya wananchi.

Mkutano huo unaojikita katika usalama wa taifa, miundombinu ya kisiasa, maguezi ya uchumi na kupambana na ukame, umeendeshwa kwa pamoja na rais Framajo, na wenyeviti wenza, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May.

Guterres amesema ukame ndio  "kipaumbele kikubwa" kwa Somalia na kuomba nyongeza ya Dola milioni 900 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ili kukabiliana na janga hilo kabla halijageuka baa la njaa. Katibu huyo mkuu amesema kiasi ya watu milioni sita nchini Somalia wanahitaji msaada au karibu nusu ya wakazi wote. Umoja wa Mataifa ulisema wiki iliyopita kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, Somalia itakuwa na watoto wenye utapiamlo takribani milioni 1.4.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na katibu mkuu wa UN Antonio GuterresPicha: Imago/Photothek/xIngaxKjerx

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo na ameeleza kwamba, "Somalia inahitaji msaada wa haraka kutoka jumuiya za kimataifa ili kutimiza malengo yake ya upatikanaji wa amani na ustawi. Na kwa mantiki hii tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisadia kikamilifu Somalia katika utekelezaji wa usanifu wa usalama wa Somalia ikiwemo ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AMISOM."

Waziri Mkuu May ameuambia mkutano huo kuwa sasa Somalia inalo "dirisha muhimu la fursa" chini ya rais Farmajo ya kudhibiti usalama wake na kuimarisha uwezo wake wa kiuchumi.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, rais wa Uganda Yoweri Museveni, mawaziri wakuu wa Ethiopia na Uturuki, na mawaziri wa kigeni wa Misri, Ujerumani, Uholanzi na Qatar.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW