1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa usalama kuanza Munich

17 Februari 2023

Mkutano wa kimataifa wa usalama unaofanyika kila mwaka mjini Munich unang'oa nanga leo, ukiwaleta pamoja viongozi wa ulimwengu kabla ya kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

USA | Antony Blinken
Picha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

Akizungumza kabla ya mkutano huo, mwenyekiti Christoph Heusgen alisema washiriki watapambana na suali la jinsi utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria unaweza kuheshimika. Heusgen aliuliza, na hapa namkuu, katika siku za usoni, kutakuwa na utaratibu ambapo nguvu ya sheria inatawala, au kutakuwa na utaratibu ambao sheria ya wenye nguvu Zaidi itatawala?

Mahusiano ya Marekani na China pia yatawekwa kwenye darubini kwenye mkutano huo wa siku tatu, huku mivutano ikipaa juu zaidi baada ya Washington kudungua kile ilichodai kuwa ni puto la kijasusi la China lililoruka katika anga ya Marekani.

Soma pia: Makamu wa rais wa Marekani kufanya mazungumzo na viongozi wa Ulaya katika mkutano wa usalama wa Munich

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron watazungumza katika hafla ya ufunguzi, itakayoangazia vita vya nchini Ukraine. Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris na Waziri wa Mambo ya Kigeni Antony Blinken, mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi na mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltnberg pia wanahudhuria.

Washirika wa NATO waahidi msaada zaidi kwa UkrainePicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP

Wakati ukifanyika ikiwa ni siku chache tu kabla ya Februari 24 ambayo ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Moscow ilipotuma wanajeshi wake nchini Ukraine, mzozo huo utakuwa mada kuu, huku waziri wa mambo ya kigeni Dymitro Kuleba akiiwakilisha Ukraine.

Washirika wa Ukraine kutoka nchi za magharibi, wakiongozwa na Marekani, wameipa kiasi kikubwa cha silaha na kuahidi nyingine chungu nzima, zikiwemo vifari vikubwa vya kivita ambavyo Kyiv imevitafuta kwa muda mrefu ili kupambana na mashambulizi ya Urusi. Nico Lange, mtaalamu kuhusu mzozo wa Ukraine kutoka Mkutano wa Usalama wa Munich anasema

Kikubwa kwa sasa ni kuwa Urusi imekabiliana na zana ambazo Ukraine inatumia. Hasa upande wa kusini, ambako kuna eneo dogo lililokamatwa na Urusi. Urusi ina udhibiti wa miundombinu, nyenzo za miundombinu nje ya uwezo wa Ukraine. Na bila shaka, ili kuandaa uwanja wa mapambano kwa shambulizi, ili kulikomboa eneo hilo, Ukraine inahitaji zana zaidi.

Rais Volodymyr Zelensky sasa anaongeza miito kwa nchi za magharibi kumpa ndege za kivita, ijapokuwa washirika wa Ukraine wamekuwa watulivu mpaka sasa kuhusu suala hilo

Soma pia: Blinken kuzuru Ulaya katikati mwa fukuto la mzozo na China

Lakini uamuzi wa Berlin kuruhusu vifaru vya Leopard vinavyoetengenezwa Ujerumani kupelekwa Ukraine – baada ya wiki kadhaa za kusita – umeongeza matumaini mjini Kyiv kuhusu uwezekano wa kupelekwa silaha zaidi katika siku za usoni.

Maafisa wa NATO wiki hii walijadili haja ya kupekelekwa zana za kijeshi nchini Ukraine, na Uingereza na Poland zikakubali baada ya viongozi wao kukutana jana kuwa msaada unapaswa kuimarishwa.

Maafisa wa Marelani wameishauri Kyiv kupambana na mashambulizi yoyote hadi pale zana mpya za Marekani zitakapokuwa tayari na mafunzo kutolewa.

afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW