1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kuboresha kilimo Afrika wafanyika Uganda

10 Januari 2025

Kongamano la CAADP kuhusu ukuzaji wa kilimo jumuishi Afrika limefanyika Kampala, likihusisha mataifa 49 kujadili mikakati ya kuboresha usalama wa chakula na mageuzi ya sekta ya kilimo, kuanzia uzalishaji hadi lishe bora.

Uganda | CAADP-Agrargipfel
Kikao cha kujadili ushiriki wa wanawake na vijana katika kilimo.Picha: Lubega Emmanuel/DW

CAADP imekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo kati ya serikali za Afrika na wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kujitosheleza kwa chakula ifikapo mwaka 2063.

Tangu kuanzishwa kwake, mafanikio kadhaa yamepatikana, hasa kupitia Azimio la Malabo la 2014. Hata hivyo, changamoto kama vile uzalishaji duni, gharama za juu za maisha, na uhaba wa chakula zinaendelea kudhoofisha maendeleo. 

Wanawake na vijana, ambao ni nguzo muhimu za uzalishaji, wanahitaji kupewa nafasi kubwa katika sekta ya kilimo. Hii ni pamoja na umiliki wa ardhi na fursa za kifedha ambazo zimekuwa changamoto kwao. 

Kwa nini Afrika lazima iimarishe kilimo cha kisasa ?

01:52

This browser does not support the video element.

Katika majadiliano hayo, Wanjiku Wanjohi wa Shirika la Oxfam alisema: "Wanawake hawawezi kuendesha kilimo ipasavyo kwenye ardhi ambayo si yao licha ya kuwa wao ndiyo wazalishaji wakuu." 

Soma pia: Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika lahitimishwa Tanzania

Emmanuel Makula kutoka Mwanza, Tanzania, aliongeza: "Vijana na wanawake wanahitaji kuwezeshwa kupitia ufadhili wa kifedha ili wachangie katika kuinua kilimo. Hii itasaidia hata kupunguza gharama za maisha na fursa za kazi." 

Umuhimu wa CAADP

Meja Jenerali David Kyomukama, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Uganda, alieleza kuwa kongamano hili lina umuhimu mkubwa katika kukuza uzalishaji na masoko ya kilimo barani Afrika, jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama za maisha.

Kongamano hili linatarajiwa kufikia kilele chake katika kikao cha marais wa mataifa ya Afrika, ambapo maazimio mapya yatapitishwa. 

Kongamano hili limeandaliwa na Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na mashirika ya maendeleo barani Afrika, likiwa na matumaini ya kuchochea mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW