1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mkutano wa kuijenga upya Ukraine kufungua pazia mjini London

21 Juni 2023

Uingereza hii leo Jumatano itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa kukusanya nguvu za kuijenga upya Ukraine iliyoharibiwa kwa vita.

Uharibifu wa vita
Vita vimeleta uharibifu mkubwa nchini Ukraine Picha: Sameer Al-Doumy/AFP

Zaidi ya wajumbe 1,000 kutoka nchi washirika, wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa na wawakilishi wa sekta binafsi watautumia mkutano huo kujadili njia za kupata fedha za kuisaidia Ukraine kusimama tena. 

Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika mjini London ni sehemu ya juhudi pana ya kimataifa ya kuipiga jeki Ukraine ambayo imeshuhudiwa uharibifu usio kifani tangu Urusi ilipoivamia nchini hiyo zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Katika siku ya kwanza Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak anatarajiwa kutangaza msaada mkubwa wa kifedha kwa Ukraine ikiwemo kitita cha dola milioni 306 pamoja na dhamira ya kutanua uwekezaji wake nchini Ukraine.

Vilevile Uingereza inataka kuiwekea dhamana Ukraine yenye thamani ya dola bilioni 3 ili taifa hilo lipatiwe mkopo na Benki ya Dunia kutekeleza mipango ya kujijenga tena baada ya uharibifu uliotokana na vita.

Uingereza inataka kuivutia sekta binafsi nchini Ukraine 

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akiwa na rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine Picha: Stefan Rousseau/WPA Pool/Getty Images

Uingereza imekuwa miongoni mwa wafadhili wakubwa wa Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo mapema mwaka jana. Waziri Mkuu Sunak anatumai mkutano huo utaichochea sekta binafsi katika kuijenga upya Ukraine.

Sehemu ya hotuba ya Sunak iliyotolewa na ofisi yake inaonesha atawarai washiriki wa mkutano huo kuendelea kuiunga mkono Ukraine bila kuchoka kwenye mapigano dhidi ya Urusi. 

Baada ya mwaka mzima wa vita nchini Ukraine, waziri mkuu Sunak anatumai mkutano huo utaivutia pia sekta binafasi kutumia rasilimali ilizonazo kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo. Hata hivyo changamoto kubwa itakuwa ni kuwashawishi wawekezaji juu ya usalama wa mitaji yao nchini Ukraine.

Uingereza inapanga kutangaza muongozo wa kulinda  mitaji ya wawekezaji wa sekta binafsi kama njia ya kuongeza imani yao kufanya biashara na Ukraine.

Zelensky asema Ukraine iliyojengwa upya ni dhamana ya usalama 

Mapigano bado ni makali kwenye uwanja wa vita Picha: Oleksandr Ratushniak/REUTERS

Rais Volodmyr Zelensky amesema mkutano huo utakuwa nafasi ya kutangaza azma ya nchi hiyo ya kusisimama tena baada ya vita. Akizungumza kupitia hotuba ya kila siku kwa taifa Zelenksy amesema:

"Ukraine iliyojengwa upya, iliyofanyiwa mageuzi na iliyo imara ni dhamana ya usalama. Ni kinga dhidi ya kitisho chochote cha Urusi na ulinzi dhidi ya kutotokea tena kwa ufedhuli wa Urusi. Kwenye mkutano wa London nitawasilisha sehemu ya falsafa yetu ya mageuzi nchini Ukraine. Picha kamili ya hilo itawasilishwa baadaye mwezi huu ikiwemo humu nchini" amesema rais Zelensky.

Kiongozi huyo atauhutubia mkutano huo kwa njia ya video.  Inatarajiwa Marekani itautumia mkutano huo kutangaza awamu nyingine ya msaada kwa Ukraine.

Kwa upande Ujerumani imesema kazi ya kuijenga upya Ukraine itakuwa "changamoto kubwa" lakini serikali mjini Berlin imejipanga kushiriki juhudi hizo.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema kwa mwaka 2022 pekee Ukraine imepoteza asilimia 29 ya pato lake la ndani na mfumuko wa bei umefikia asilimia 27.

Benki ya Dunia inakadiria nchi hiyo inahitaji kiasi Euro bilioni 400 ili kujijenga tena katika kipindi cha muongo mmoja unaokuja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW