Mkutano wa kuisaidia Syria waanza mjini Brussels
24 Aprili 2018Umoja wa ulaya unataraji pia kuzipatia pia Urusi, Uturuki na Iran nafasi ya kuendeleza juhudi za amani. Mnamo wakati ambapo vita vya Syria vimeingia katika mwaka wake wa nane, Umoja wa ulaya umezialika serikali 85 na mashirika yasiyomilikiwa na serikali kukusanya fedha kwaajili ya misaada ya kiutu, ujenzi mpya na juhudi za kufichua mabomu katika miji iliyoteketezwa kwa vita.
"Kugharimia misaada,si rahisi" amesema Robert Beer katika mkutano wa shirika la misaada la CARE International. Lakini gharama ni sehemu tu ya picha -mtindo wa kuzuwiliwa makusudi misaada ndani nchini Syria inabidi ikome na watumishi wa mashirika ya misaada waruhusiwe kuwafikia raia" amesema Robert Beer katika taarifa yake.
Mkutano huu, wa tatu wa wafadhili kuwahi kuitishwa baada ya ule wa mjini London mwaka 2016 na mwaka jana mjini Brussels, unaweza kusaidia kurejesha nguvu za umeme na mitambo ya maji katika baadhi ya miji iliyoharibiwa kutokana na opereshini za nchi za magharibi kuwatimua wanamgambo wa itikadi kali wa IS.
Lakini sehemu kubwa ya fedha hizo huenda zikawahudumia wakimbizi wa Syria walioko nchi za nje na mamilioni waliotawanyika nchini Syria kwenyewe ikiwa ni pamoja na watu 160.000 waliotoroka opereshini za kijeshi za wiki sita zilizopita zilizoendeshwa na washirika wa Syria, Urusi, mashariki mwa Ghouta, karibu na Damascus.
Lengo la kukusanywaa kiasi cha dala bilioni sita linalingana na kiwango cha fedha zilizokusanywa mwaka jana, lakini maafisa wanasema wamepania kuona kiwango hicho kinapindukia.
Ujenzi mpya wa miji iliyoteketezwa mfano wa Aleppo unaweza kugharimu mabilioni ya dala, hata hivyo hautaweza kuanza kabla ya madola makuu yanayohusika na vita kukubaliana kuhusu kipindi cha amani cha mpito baada ya utawala wa rais B ashar al Assad.Taarifa ya umoja wa ulaya imesema.
Miongoni mwa wafadhili wakubwa ni pamoja na Umoja wa ulaya, Marekani , Norway na Japan.
Serikali zinategemea pia kuwatuma mawaziri mkutanoni huku Uturuki ikithibitisha itawakilishwa na naibu waziri mkuu Recep Akdag na Iran nayo pengine ikawakilishwa na waziri wa mambo ya nchi za nje Javad Zariff-hayo lakini ni kwa mujibu wa maafisa wa umoja wa ulaya.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Serggei Lavrov pia amealikwa lakini haijulikani bado kama atahudhuria. Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de Mistura aliyekutana na Lavrov April 20 iliyopita nae pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa wafadhili mjini Brussels.
Kutohudhuria mkutanoni mwaka jana wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka Urusi, Uturuki na Marekani pamoja pia na shambulio ya gesi za sumu nchini Syria ni visa avilivyogubika juhudi za mkutano huo kusaidia kuumaliza mvutano kati ya makundi ya waasi wanaompinga Assad,wanamgambo wa itikadi kali ya dini ya kiislam,wanajeshi wa syria na vikosi vya kigeni.
Safari hii mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya umoja wa ulaya bibi Federica Mogherini anazisihi pande zote tatu, Urusi, Iran na Uturuki-wanaochangia moja kwa moja katika vita vya Syria, waunge mkono jzuhudi za kufikiwa makubalino ya kudumu ya kuweka chini silaha na kuruhusu misaada ya kiutu iwafikie raia pamoja na kuhamishwa majeruhi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu