Mkutano wa LDC mjini Istanbul
9 Mei 2011Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, katika hotuba yake ya ufunguzi, ametoa wito wa kuwekeza katika nchi zenye maendeleo duni, maarufu pia kama kundi la LDC. Amesema, uwekezaji katika nchi hizo masikini utasaidia pia kufufua uchumi wa kimataifa. Baadae aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa yeye amekwenda mkutanoni na ujumbe mmoja tu: "Nchi zenye maendeleo duni, zitakuja kuwa muhimu kabisa katika wimbi la maendeleo." Akasisitiza kuwa haombi msaada, bali anatoa wito wa kuwekeza katika nchi hizo masikini. Uwekezaji huo utaweza kuzinufaisha nchi hizo masikini pamoja na uchumi wa kimataifa. Kwani mafanikio katika nchi zenye maendeleo duni, vile vile humaanisha mafanikio kwa kila mmoja.
Ban amesema, wakati umewadia kubadili mtazamo wetu. Badala ya kuzitazama nchi zenye maendeleo duni kama mataifa yalio fukara, nchi hizo 48 zitambuliwe kama ni nchi zenye uwezo mkubwa. Muhimu kabisa ni kusaidia kilimo, kwani asilimia 70 ya umma katika nchi hizo, hufanya kazi katika sekta ya kilimo. Na hivi sasa nchi hizo zinakabiliwa na kitisho cha kutokea mzozo wa chakula.
Ughali wa maisha ni kitisho
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ban, maendeleo yaliyopatikana hadi sasa ni madogo mno na idadi ya nchi zinazoorodheshwa na Umoja wa Mataifa kama nchi zenye maendeleo duni, imefikia 48. Huo ni mwongezeko wa takriban maradufu, tangu utaratibu wa kuorodhesha nchi hizo kuanzishwa katika miaka ya 1970. Nchi 33 ni kutoka bara la Afrika,14 barani Asia na Haiti, nchi pekee kutoka ulimwengu wa nchi za Magharibi. Jumla ya watu milioni 885, wanaishi katika nchi zenye maendeleo duni na asilimia 75 ya umma huo, unaishi kwa kutumia chini ya dola 2 kwa siku.
Miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa kuorodhesha nchi kama hizo, ni pato la jumla la taifa lisilopindukia dola 905 kwa mwaka kwa kila mkaazi; kiwango kikubwa cha vifo vya watoto wachanga; shida ya kupata elimu pamoja na ukosefu wa usalama wa chakula na uchumi. Matatizo ya chakula na uchumi ndio yaliyochochea mapinduzi ya hivi karibuni katika ulimwengu wa Kiarabu. Hata katika nchi nyingi masikini, kuongezeka upya kwa bei za vyakula kumechochea ghasia za kiuchumi na kijamii, na hiyo ni mada kuu ya viongozi wanaokutana mjini Istanbul.
Mwandishi: P.Martin/afpe,rtre
Mhariri: M.Abdul-Rahman