1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa kufanyika mjini Montreal, Canada

Josephat Charo17 Novemba 2005

Katika muongo uliopita mataifa mengi yalisaini mkataba wa umoja wa mataifa wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Lengo lao kubwa ni kutafuta njia za kupunguza na kukabiliana na ongezeko la uoto duniani. Sekretariati ya umoja wa mataifa ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa iliandaa mkutano na waandishi habari uliofanyika jana katika ukumbi wa Redio Deutsche Welle hapa Bonn.

Alama itakayotumiwa katika mkutano wa Montreal nchini Cananda
Alama itakayotumiwa katika mkutano wa Montreal nchini Cananda

Mkutano wa kilele wa umoja wa mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa umepangwa kufanyika mjini Montreal nchini Canada kuanzia tarehe 28 mwezi huu hadi tarehe 9 mwezi ujao wa Disemba. Mkutano huo ni wa kihistoria, sio tu kwa sababu wanachama wa kamati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa wanakutana kwa mara ya 11, lakini pia mwaka huu wa 2005 ni mwaka unaoashiria kuanza kutekelezwa kwa mkataba wa Kyoto.

Kwa mara ya kwanza mkutano huo utakuwa na vikao vya wanachama waliosaini mkataba wa Kyoto na wanachama wa kamati ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mkutano huo utakuwa wa kwanza mkubwa tangu kusainiwa mkataba wa Kyoto mwaka wa 1997 na unatarajiwa kuwakusanyisha wajumbe kati ya elfu 8 na elfu 10. Mkutano huo pia umewavutia wafanyabiashara wengi kutoka Ulaya na Marekani kufuatia kuanza biashara ya gesi zinazotoka viwandani na teknolojia ya kuzisafisha kama chombo cha kuboresha maendeleo endelevu na kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa.

Umoja wa mataifa unatambua juhudi za serikali mbalimbali duniani katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Unatambua pia kwamba mifumo ya hali ya hewa ni raslimali muhimu kwa mataifa yote ulimwenguni ambayo ustawi wake unaweza kuathiriwa na gesi ya dioksidi ya kaboni na gesi nyengine kutoka viwandani na sehemu tofauti.

Katika mkataba wa UNFCCC serikali hukusanya na kubadilishina habari juu ya gesi kutoka viwandani, sera za kitaifa na njia zilizo salama. Huzindua mikakati ya kitaifa ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kutoa udhamini wa kifedha na kiteknolojia kwa mataifa yanayoendelea. Mataifa haya pia yamekubaliana kushirikiana kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Marekani itashiriki katika mkutano wa Montreal ijapo inapinga mkataba wa Kyoto na inatarajiwa kuhimiza kuanzishwa kwa teknolojia mpya itakayotumiwa kupunguza kiwango cha gesi kutoka viwandani. Lakini kuna mipango yoyote ya kulisaidia bara la Afrika kuweza kuanzisha teknolojia yake?

Bwana Sergey Konokov, afisa wa sekretariat ya umoja wa mataifa mjini Bonn, alisema kwamba kila mtu anafahamu teknolojia ni muhimu kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Mkutano wa Montreal utajadili njia za kuboresha nyenzo za kubadilishana teknolojia na vipi zitakavyotekelezwa. Matokeo mazuri yanayotarajiwa mjini Montreal ni kunzishwa kwa oparesheni mpya. Kupitia misaada ya mataifa yanayoendelea, teknolojia mpya inaweza kuzifikia nchi hizo, hususan barani Afrika, ikiwa zinataka kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Bwana Sergei aliitaja Ujerumani kama taifa la pekee barani Ulaya lililofaulu kupunguza kiwango cha gesi hatari katika anga yake. Imeweza kupunguza kiwango hicho kwa asilimia 18.2 ikilinganishwa na asilimia 21 inayotakikana na mkataba wa Kyoto. Uhispania kwa upande wake imetajwa kama taifa ambalo limeshindwa kutimiza maagizo ya mkataba wa Kyoto. Kiwango cha gesi kiliongezeka kufikia asilimia 41.7 badala ya asilimia 15 inayotakikana na mkataba huo.

Inakadiriwa kuna wakimbizi wa mazingira takriban milioni 25 duniani. Je mkutano wa Montreal utajadili mambo gani kuwasaidia na kuzuia kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi hawa?

Bwana Sergei alisema katika mkutano huo jambo moja muhimu litakalojadiliwa ni mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Ni katika mtazamo huu ambapo uamuzi unatakiwa kufanywa wa kuwasaidia wakimbizi wa mazingira kuweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayowaathiri maisha yao ya kila siku katika mazingira wanamoishi.

Ni vigumu lakini kutarajia kwamba matatizo yote yatapata ufumbuzi kesho au baada ya kumalizika kwa mkutano wa Montreal, lakini mkutano huo utatoa mwelekeo wa kukabiliana na tatizo hili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW