1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ujerumani kuingia Syria

30 Novemba 2015

Mkutano wa kille kuhusu mabadiliko ya tabianchi mjini Paris,mzozo wa Syria na wakaazi wa Hamburg kupinga kuandaa michezo ya Olympik ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Rais Hollande wa Ufaransa akimkaribisha rais Obama wa Marekani katika mkutano wa kilele wa Mabadiliko ya Tabianchi mjini ParisPicha: Reuters/C. Hartmann

Tuanzie na mkutano wa kilele kuhusu mabadiliko ya tabia nchi mjini Paris.Gazeti la Badische Neueste Nachrichten,linaandika:"Tangu zama za zama na katika mabara yote ya dunia,mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakisababisha madhara tangu ya kisiasa mpaka ya kijamii;maafa yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ndio chanzo cha kutoweka warumi ,watu wa jamii ya-maya na wale wa jamii ya Inka.Mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi unapoanza hii leo mjini Paris,viongozi wa dunia wakijiweka lengo la kufikia makubaliano ya kupunguza kiwango cha moshi wa sumu duniani ili kuweza kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binaadamu,wasisahau tu viongozi hao kuangalia yaliyomo ndani ya madaftari ya historia na kuyachukulia kama onyo na wajib kwa wakati mmoja."

Matarajio ya kufanikiwa mkutano wa kilele wa Paris

Gazeti la Mittelbayerisch Zeitung linahisi hifadhi jumla ya mazingira si kazi rahisi.Gazeti linaendelea kuandika:"Hifadhi jumla ya mazingira ni kazi ngumu.Watu wanabidi wajiandae kukabiliana na upinzani mkubwa,kuvumilia pingamizi,kutafuta washirika wepya na muhimu zaidi kuliko yote kutoachana na lengo watu walilojiwekea;Watu wanabidi wafanikiwe kupunguza kwa nyuzi joto mbili kiwango cha hali ya joto kilichosababishwa na binaadam wenyewe,hadi ifikapo mwisho wa karne hii na kubuni hali ya kiuchumi na maisha itakayoambatana kwa namna fulani na usafi wa mazingira.Kinachopiganiwa hapo si chochote chengine isipokuwa mustakbal wa sayari yetu ya dunia.Licha ya pingamizi zilizoko,mkutano wa kilele wa Paris una nafasi nzuri ya kuleta tija."

Mapambano dhidi ya IS

Gazeti la Rhein-Necker-Zeitung linazungumzia uamuzi wa Ujerumani kutuma wanajeshi nchini Syria.Gazeti linajiuliza:"Adui ni nani?Ni wapiganaji wa dolsa la kiislam peke yao?Na wale wanaoitwa waasi wanaofuata msimamo wa wastani je?Lengo la kutumwa wanajeshi ni nini?Kwa namna gani Syria na baadae Iraq zinaweza kukombolewa?Masuala yote hayo bado hayana majibu.Na bila ya majibu,haitakuwa busara kuelekea Syria.Kwasababu matokeo yake yatakuwa kuzidisha vurugu tu.

Hamburg yasema La

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na kura ya maoni ya Hamburg kama wananchi wanapendelea kuandaa michezo ya Olympic ya msimu wa kiangazi mwaka 2024.Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linaandika:"Makadirio yote ya kutia moyo hayakusaidia kitu;Wakaazi wa Hamburg wameizika katika mto Elbe ndoto ya kuandaa michezo ya Olympik.Kwisha.Bahati mbaya lakini sio mwisho wa dunia.Na wanaspoti hawapaswi kujiangalia wawo kuwa ndio sababu ya kushindwa huko.Bila ya shaka wimbi la wakimbizi limechangia hali hiyo na mashambulio ya kigaidi ya Paris yanawafanya watu wazidi kuwa na hofu.Lakini kura ya la ya wakaazi wa Hamburg imesababishwa na kitu chengine kabisa-Ulimwengu wa viongozi wa michezo wanakabwa na matatizo ya kila aina.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW