1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

310510 ICC Baschir Kampala

Josephat Nyiro Charo31 Mei 2010

Mkutano unaolenga kuufanyia mageuzi mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, umeanza leo mjini Kampala nchini Uganda. Mkutano huo unatoa nafasi ya kwanza kutoa mapendekezo ya mageuzi

Luis Moreno Ocampo, muendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICCPicha: AP

Mahakama ya ICC inakabiliwa na uchunguzi muhimu katika mkutano wa Kampala huku tathmini ikitarajiw akufanywa kuhusu utekelezaji wa mkataba wa Roma na ufanisi uliopatikana tangu kuanzishwa mahakama ya ICC

Tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2002 mahakama ya ICC imejihusisha sana na bara Afrika, ingawa ofisi ya muendesha mashtaka mkuu inafanya uchunguzi pia nchini Afghanistan, Colombia, Georgia na katika maeneo ya Wapalestina. Mahakama hiyo pia inaendesha uchunguzi wake nchini Guinea na Ivory Coast. Nchi 30 kati ya 53 wanachama wa Umoja wa Afrika zimesaini mkataba wa Roma kuitambua mahakama ya ICC.

Afrika inachukua nafasi ya pili kwa kuwa na nchi nyingi zilizouidhinisha mkataba huo, lakini mahakama ya ICC imekuwa mara kwa mara ikifuatilia kesi za uhalifu wa kivita barani Afrika, dai ambalo muendesha mashataka mkuu wa mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo, amelipinga kwa maneno makali.

"Sitafuta ushauri wa kutofungua kesi barani Afrika, bali nitafuata sheria. Naamini wazo kwamba tunalionea bara la Afrika ni propaganda ya kisiasa ya wakandamizaji. Sitabadili sheria kwa sababu ya propaganda ya kipuuzi."

Katika mkutano wa mjini Kampala mahakama ya ICC inakabiliwa na uchunguzi muhimu kupima ni kwa umbali gani imeweza kufaulu katika kutekeleza kazi yake kwa mujibu wa mkataba wa Roma. Pengine ufanisi mkubwa wa mahakama hiyo katika kipindi chake cha miaka 8 ni kutangaza waranti wa kukamatwa rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir.

Muendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC, Luis Moreno Ocampo, alitangaza waranti huo mnamo Machi 4 mwaka jana, akisema kwamba kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka saba ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na mateso.

Uamuzi wa mahakama ya ICC ulisababisha hali ya wasiwasi, hususan miongoni mwa wakaazi wa jimbo linalokabiliwa na mzozo la Darfur magharibi mwa Sudan. Serikali ya Sudan iliyafukuza mashirika yote 11 ya misaada na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji safi ya kunywa na dawa, huku wakimbizi wakiachwa wajisimamie wenyewe. Je, waranti huo umekwamisha juhudi za kutafuta amani nchini Sudan? Mashirika ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International na Human Rights Watch yameunga mkono waranti huo dhidi ya rais Bashir, huku raia wa Darfur wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu.

Mkutano wa mjini Kampala unalenga kufikia makubaliano ya kupanua mamlaka ya mahakama ya ICC kuchunguza uchokozi unaofanywa na serikali kama uhalifu kwani katika mkataba wa sasa, muendesha mshtaka hana mamlaka ya kuchunguza uchokozi wa aina yoyote ile. Nchi zote zilizosaini mkataba wa Roma zinaunga mkono kwamba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ndilo linalotakiwa kuwa chombo cha kwanza kuamua ikiwa nchi fulani imeichokoza nchi nyengine.

Rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: AP

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliwasili jana mjini Kampala na anatarajiwa pamoja na rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kuuhutubia mkutano huo. Hapo jana Ban Ki Moon alishiriki kwenye mchuano wa kandanda kati ya wajumbe wa mkutano wa Kampala na wahanga wa mizozo nchini Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Timu ya bwana Ban iliyoitwa, Justice, yaani haki, ilishindwa na timu ya rais Museveni kwa bao moja kwa bila.

Mkutano wa mahakama ya ICC unatarajiwa kumalizika hapo Juni 11 mwaka huu na wajumbe watatoa tamko kuhusu ushirikiano kati ya mahakama hiyo na vyombo vya usalama vya nchi wanachama.

Mwandishi: Nyiro Charo, Josephat/Duckstein, Stefanie/ZPR

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW